Na Scolastica Msewa.
PWANI.
Benki ya NMB imechangia shilingi Milioni 30 ikiwa ni katika kufanikisha Uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru utakaofanyika Aprili 2 ,2025 kwenye Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha Mkoani Pwani ambapo wahudhuriaji 16,000 wanatajiwa katika uzinduzi huo.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Benki ya NMB, Tawi la Mlandizi, William Marwa, wakati wa kongamano la Vijana la kuhamasisha Umuhimu wa Kushikriki Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 linalofanyika kwa siku mbili katika Ukumbi wa Bertil Merlin, Kibaha Sekondari, mkoani Pwani ambapo mchango huo utasaidia maandalizi ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru.
Marwa amesema kwa miaka kadhaa benki ya NMB imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi kwa kujikita zaidi kwenye miradi ya elimu, afya na majanga mbalimbali yanayoipa nchi ya Tanzania.
“Tunatambua kuwa ni kupitia jamii ndipo wateja wengi wetu wanapotoka, kwa hiyo kurudisha sehemu ya faida kwa jamii ni yutaratibu wetu.Kwa maana hiyo NMB tumeamua kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, kwa kuchangia jumla ya thamani ya Shilingi Milioni 30,” amesema Marwa
“Kupitia shughuli hii ya kitaifa, tunawashauri vijana kutumia fursa hii, kuelewa historia ya taifa lao pamoja na Mwenge wa Uhuru kama kielelezo muhimu cha utaifa.”
Amebainisha kuwa benki ya NMB imejikita katika maendeleo ya elimu, misaada ya hali na mali katika nyakati ngumu kama majanga.
“Kwa mwaka 2025, NMB imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 6.4 kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya jamii, ikiwemo kusaidia sekta ya afya na elimu.Kiasi hiki kinatufanya kuwa benki ya kwanza katika kuchangia maendeleo kuliko benki yoyote hapa nchini.”
Amesema benki hiyo inatambua nafasi ya Mwenge wa Uhuru katika kuchochea maendeleo na uzalendo miongoni mwa Watanzania, wakiwamo vijana.
“Kwa taarifa tu, NMB ndiyo benki inayoongoza nchini kwa kuwa na matawi 241, ATM zaidi ya 720, NMB Wakala zaidi ya 50,000 pamoja na idadi ya wateja zaidi ya Milioni 8.7, idadi ambayo ni hazina kubwa ukilinganisha na benki nyingine, ikiwa imezifikia wilaya zote nchini.”
Amesema mchango huo ni sehemu ya dhamira ya NMB katika kusaidia shughuli za kijamii, hususani kwa vijana na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
"Tumeona ni muhimu kuunga mkono jitihada hizi kwani Mwenge wa Uhuru unaashiria mshikamano na maendeleo ya nchi.Vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuyatekeleza maono haya kwa vitendo."
Akizindua kongamano hilo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta ambaye alikuwa ni mgeni rasmi, amesema serikali inatambua umuhimu wa kundi la vijana katika kuleta mageuzi ya kijamii na kiuchumi kutokana na ari, nguvu na ubunifu walionao.
“Kwa kutambua hilo serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikitoa kipaumbele kwa vijana kupata elimu na makuzi bora, kuwapa fursa ya kupata mikopo ya asilimia 10 kupitia Halmashauri na Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (Build Better Tomorrow – BBT),” amesema Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta na kuongeza:
“Vile vile kongamano hili limeandaliwa katika mtazamo wa kuwajengea uwezo vijana juu ya umuhimu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika kujenga udugu, utu, uzalendo, uwajibikaji katika usimamizi wa shughuli za maendeleo na kutambua fursa za kiuchumi.
Mratibu wa kongamano hilo Omari Punzi amesema Katika kongamano hilo, vijana wamepata nafasi ya kujadili mada mbalimbali kama vile: Historia na Falsafa ya Mwenge wa Uhuru (Uzalendo, Itifiki na Maadili), Fursa za Kiuchumi zinazotokana na Mwenge wa Uhuru, Umuhimu wa Kushiriki katika Shughuli za Utunzaji wa Mazingira,
Amesema umuhimu wa Kushiriki katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Stadi za Maisha na Stadi za Kazi, Malezi na Makuzi kwa vijana, Afya na Afya ya Uzazi.
Uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru Kibaha utaambatana na miradi mbalimbali ya maendeleo itakayozinduliwa, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu, miradi ya afya na elimu, ambayo yote yanatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wananchi wa mkoa wa Pwani.
0 Comments