Na Scolastica Msewa,
PWANI.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu, Wilaya ya Rufiji CWT Mwalimu Ramadhani Dihuzi, ameomba serikali iwajengee Walimu wanaofundisha katika shule zilizopo katika maeneo ya mbuga ya Seluo wilayani Rufiji nyumba bora na imara ili wanapofanya kazi zao wawe na uhakika wa usalama na amani kwenye makazi yao ikiwa ni kwasababu ya kuwalinda na wanyama wakali ambao ni pamoja na tembo.
Amesema hayo katika Mkutano Mkuu wa pili kikatiba, katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi uliomaliza muda wake wa Chama cha CWT ulifanyika katika Ukumbi wa FDC, Ikwiriri, Wilaya ya Rufiji ukiwa ni mkutano ambapo pamoja na kujadili masuala mbalimbali, wajumbe wamepata fursa ya kuwachagua viongozi wa ngazi ya wilaya, ambao watakiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mwalimu Dihuzi alisema kuna walimu ambao wanafanya kazi karibu na mbuga za Seluo ambako muda wote wanyaka kama tembo wanafika kwenye makazi yao hivyo tunaomba serikali kujenga nyumba Bora na imara ili kuhakikiasha usalama wa Walimu huko maeneo ya mbugani.
Alisema viongozi wa CWT Rufiji kwa ushirikiano mkubwa wa serikali wanashughulikia maslahi ya Walimu kama vile madaraja kupanda kwa wakati, ujenzi wa nyumba bora za walimu hususani wale wanaoishi kandokando au pembezoni mwa Wilaya ya Rufiji.
“Kwa mfano kuna walimu ambao wanafanya kazi karibu na mbuga za Seluo wakati wote tembo wanafika kwenye makazi yao, kwa hiyo sisi tunakwenda kuihimiza ili usalama uwepo kwenye makazi yao,” alisema.
“Wito wangu, walimu wote tushikamane Sasa hivi tuna mchakato wa ubadilishaji wa mtaala, walimu wengi hawajapata mafunzo endelevu nay a kutosha ili waende sambamba na mabadiliko ya mtaala, hili tunaomba wizara iliangalie.Muda mwingine vitabu vinakuja kwa kuchelewa au vinakuwa tayari lakini vipo mtandaoni na kuna shule nyingine zipo kwenye maeneo ambayo yanachangamoto ya mtandao.
Mabadiliko haya yaende sambamba na utoaji wa vitendea kazi na utoaji wa semina kwa walimu,” alisisitiza Mwenyekiti wa CWT, Wilaya ya Rufiji, Mwalimu Ramadhan Dihuzi.
Alisema katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi uliomaliza muda, ukiwa na jukumu la kupitia taarifa za utendaji kazi, taarifa za fedha kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita na kufanya uchaguzi wa viongozi wote wa ngazi ya wilaya, watakokiongoza chama kwa muda wa miaka mitano (2025 hadi 2030.)
“Walimu tuna changamoto nyingi katika masuala ya haki zetu, ndani ya miaka mitano ijayo kitu tunachokwenda kukifanya ni kuhakikisha kwamba tunadai madai yote ya walimu.Kwa mfano kuna walimu wanadai malimbikizo yao ya mishahara, kwa hiyo tutakwenda kufanya majadiliano na serikali ili kuhakikisha madeni hayo yanalipwa,” alisema Mwenyekiti wa CWT, Wilaya ya Rufiji, Mwalimu Dihuzi.
Mkuu wa wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Luteni Kanali, Fredrick Komba, amewataka Chama cha Walimu Wilaya hiyo ya Rufiji CWT kujadili kwa kina katika mikutano yao mambo mbalimbali ya maadili ya Walimu na kulinda Wanafunzi dhidi ya unyanyasaji ili kuiinua na kuipaisha wilaya hiyo kielimu.
Luteni Kanali Komba, alisema mpaka sasa hajapokea kesi yoyote, na kubainisha kwamba hali hiyo inaonyesha kwamba walimu wanatekeleza majukumu yao kwa weledi lakini mkutano huo utatoa uwanja mpana wa kujadilia kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo unyanyasaji wa watoto shuleni,
“Mimi kama Mkuu wa Wilaya, nimekuwa nikifuatilia sana kupitia Wakuu wa Idara za Elimu ya Msingi, Awali na Sekondari, ili kupata taarifa kila siku kuhusu uadilifu wa walimu wetu, kwa bahati nzuri walimu wetu wa Wilaya ya Rufiji ni waadilifu, hawakiuki miiko yao,” alisisitiza.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya alisema ameonyesha kuridhishwa na utendaji kazi wa walimu katika wilaya hiyo, huku akipongeza mafanikio makubwa ambayo yamepatikana ikiwa ni pamoja na walimu kupatiwa utatuzi wa changamoto mbalimbali.
Kando ya hayo, DC Komba alisema kuwa hamasa na mwitikio wa walimu kufanya kazi kwa weledi bila kuangalia changamoto zilizopo, vinatokana na ushirikiano wa Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mohamed Mchengerwa, ambaye mara nyingi amekuwa akitilia mkazo kwenye suala la kuleta mapinduzi ya fikra kwa wananchi wa Wilaya ya Rufiji, ambayo yanaanzia kwenye elimu.
“Mara nyingi mheshimiwa Mbunge Mohamed Mchengerwa amekuwa akieleza kwamba falsafa yake ni kuleta mapinduzi ya fikra kwa wana Rufiji, sasa ukiangalia mapinduzi ya fikra tunaanzia kwenye elimu Kwa hiyo walimu bado wanatafsiri hiyo falsafa kwa kuhakikisha kwamba wanatimiza wajibu wao kwa njia ya kutoa maarifa kwa wanafunzi bila kujali changamoto zozote wanazokutana nazo ambazo tayari zipo kwenye madawati mabalimbali ya serikali kwa ajili ya kushughulikiwa,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Walimu mkoa wa Pwani, Mwalimu Suzan Shesha, ameishukuru serikali kuridhia kuwepo kwa kliniki ya Samia Teacher Mobile, ambayo ilikuwa na lengo moja la kusikiliza na kutatua kero za walimu nchi zima, ambapo walimu wa mkoa wa Pwani wamenufaika na uwepo wa kliniki hiyo.
“Mkoa wa Pwani ulikuwa kwenye awamu ya kwanza na walimu walisikilizwa, kituo cha kwanza kilikuwa Kibaha na kituo cha pili kilikuwa Mkuranga, changamoto zao zinaendelea kutatuliwa na nyingine zilitatuliwa palepale.Sasa hivi kilichobaki ni utekelezaji ili kusukuma yale ambayo hayajakamilika ili yaweze kukamilika.”
amesema walimu wanaendelea kushikamana na kuhimizana kufanya kazi kwa bidi huku wakiamini kwamba changamoto zao zinaendelea kutatuliwa.
0 Comments