Na AMEDEUS SOMI.
Baadhi ya vyombo vya habari vya nchi ya Morocco vimekishutumu vikali chama cha Soka Afrika CAF kwa kitendo cha kumtangaza Ademola Lookman kama mchezaji bora wa kiume wa mwaka.
Tovuti ya 365 Scores inasema gazeti la Morocco la Al-Mountakhab lilielekeza ukosoaji mkali kwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), likisema
"Kwa mara ya pili barani Afrika, Mpira wa Dhahabu umeibiwa kutoka kwa Simba wa Morocco".
Chapisho hilo pia lilishutumu kamati ya kiufundi ya CAF, yenye jukumu la kuchagua mchezaji bora wa Afrika, kwa kufanya kazi kiholela.
"Kamati inaendelea kuiba, kutengeneza, na kufanya kazi hovyo, kwa kuwadhulumu kwa makusudi Simba wa Morocco kwa mara ya pili mfululizo," gazeti hilo lilidai.
Al-Mountakhab liliisisitiza kwamba Achraf Hakimi alistahili kutawazwa mchezaji bora wa Afrika, na kutoa karipio kali kwa CAF.
Hisia hii iliungwa mkono na Al-Oumk, ambaye alichapisha maoni yake chini ya kichwa cha habari hiyo.
"Kinyume na matarajio... Mnigeria Lookman atanyakua Mpira wa Dhahabu wa Afrika wa 2024."
Achraf Hakimi beki wa Morocco na PSG |
Hakimi, ambaye hapo awali alizungumza kuhusu matumaini yake ya kushinda tuzo hiyo, bado hajajibu shutuma zinazoongezeka kuhusiana na uamuzi wa CAF wa kumpuuza tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka.
Lookman alikua mchezaji wa pili wa Nigeria kunyakua tuzo hiyo mtawalia baada ya kuikosa kwa miaka mingi kufuatia ushindi wa Victor Osimhen mwaka 2023.
Ademola Lookman akishangilia Ubingwa wa Europa na wachezaji wenzake |
Mbali na Ademola kushinda Tuzo hiyo pia kulikua na washindi wengine wengi ambapo Barbara Banda wa Zambia na Klabu ya Orlando Pride alishinda Tuzo ya Mchezaji bora wa Afrika kwa wanawake.
Sherehe za Tuzo za CAF zilifanyika katika Mji wa Marrakech nchini Morocco.
0 Comments