HEADLINES

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAVITAKA VYAMA VYA USHIRIKA KUWEKEZA


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imevitaka Vyama vya Ushirika Nchini kuwekeza katika kuanzisha na kumiliki Viwanda ili sehemu kubwa ya Viwanda hivyo  vimilikiwe na Vyama vya Ushirika pamoja na kuwa Wafanyabiashara wenye tija.

Uanzishwaji wa viwanda nchini ni miongoni mwa mikakati ya Rais Samia, katika miaka mitatu ya uongozi wake, ambapo amekuwa mstari wa mbele kuhamamisha kuinua sekta ya viwanda na uwekezaji nchini.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, ametoa rai hiyo wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa 29 wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), uliofanyika Desemba 11,  2024 Jijini Dodoma.

Amesema kuwa, kwa kufanya hivyo Ushirika utakuwa moja ya Sekta inayoongoza kutoa ajira rasmi na zisizo rasmi kwa vijana na ili kufanikisha hilo Serikali itaona uwezekano wa kutoa msamaha wa kodi kwa mashine na vipuli vyake vitakavyoagizwa na vyama hivyo kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao nchini.

Aidha, Waziri Kigahe amevihamasisha Vyama vya Ushirika kuwa na Program na mikakati ya kupambana na mabadiliko ya Tabia nchi katika maeneo yao na kuepukana na uharibifu wa Mazingira ikiwemo ukataji miti na kufanya kilimo kisicho rasmi kwani janga hilo ni kubwa na lina athari Katika shughuli hasa za kilimo. 

“Wanaushirika wanatakiwa sasa kufanya shughuli zao na kujiendesha kibiashara zaidi ili Ushirika uweze kuleta tija, kwani wanaushirika wengi ni wazalishaji wa malighafi zinazotumika na wengine kuziongezea thamani,”amesema.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania, Charles Jishuli amesema, Mkutano huo wa Ushirika kwa mwaka huu una kauli mbiu ya “Ushirika ni Biashara”, hivyo Ushirika na Wizara ya Viwanda na Biashara uko pamoja katika kuendeleza maendeleo ya Biashara nchini.

Kwa upande wake Mrajisi na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema Wanaushirika wapo katika hatua za mwisho kuanzisha Benki ya Ushirika ambayo itasaidia kutoa huduma za kifedha kwa vyama vyote vya Ushirika ikiwemo kutoa mikopo yenye riba nafuu.

Dkt. Ndiege amesema kwa sasa Sekta ya Ushirika imeendelea kuimarika, ambapo Watanzania wengi wananufaika kwa kujiunga na Vyama hivyo nchini.

#KAZIINAONGEA

Post a Comment

0 Comments