Na Mwandishi Wetu,
DAR ES SALAAM.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaamini katika usawa kwa kila mwananchi bila kujali rangi, kabila, dini au hali ya kiafya ya mtu.
Hapendi unyanyasaji wa namna yeyote ile na ndio maana Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Serikali haipendi kusikia na haitavumilia kusikia uwepo wa vitendo vya unyanyasaji kwa watu wenye ulemavu.
Dkt. Biteko amesema wale watakaojihusisha na vitendo hivyo watachukuliwa hatua kali.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam Disemba 03,2024 wakati akimwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika maadhimisho ya Siku ya watu wenye ulemavu iliyofanyika sambamba na uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa Haki na Ustawi wa Watu wenye Ualbino na Mkakati wa Taifa wa Teknolojia Saidizi kwa wenye ulemavu.
“Hatuwezi kuvumilia kuona watu wanaojihusisha na vitendo vya unyanyasaji wa watu wenye ulemavu, eti wanauza viungo vya albino, au wanafanya mauaji, nawahakikishia tutakula nao Sahani moja!,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema Kauli mbiu ya mwaka huu ni 'Kukuza uongozi kwa watu wenye ulemavu kwa ajili ya mustakabali Jumuishi na endelevu ni muafaka kwa vile inaendana na tamko la kimataifa la kukuza ufahamu wa jamii kuhusu haki za watu wenye ulemavu duniani'.
Dkt. Biteko ameongeza kuwa Serikali imeweka miongozo mbalimbali ikiwemo kutenga fedha kwa ajili ya makundi maalum ikiwemo watu wenye ulemavu.
“ Kitengo cha Ufuatiliaji na tathimini kiko ndani ya Ofisi hii ya Waziri Mkuu, kifanye ufuatiliaji kujua Ofisi na halmashauri zinavyotenga fedha kwa ajili ya makundi maalum na tupate taarifa ya ufuatiliaji wake,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Amesema haipendezi kuona tunakubaliana na kuweka maazimio ya kazi lakini utekelezaji wake unabaki katika makabrasha.
Amewaelekeza Wakuu wote wa Mikoa nchini kutekeleza mpango kazi wa haki na ustawi kwa watu wenye ualbino na kuhakikisha unatekelezwa kikamilifu na kila halmashauri nchini itenga bajeti ya ununuzi wa vifaa saidizi kwa kuzingatia uhitaji na viwango vya ubora wa vifaa hivyo na Wizara za kisetka kutekeleza Mpango na Mkakati huo kwa utaratibu uliowekwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Watu wenye ulemavu, Ridhiwan Kikwete, amesema Serikali inafanya jitihada za kuhakikisha jamii inatambua haki za kijamii kwa watu wenye ulemavu na ndiyo msingi wa kuzinduliwa kwa mkakati huo.
#KAZIINAONGEA
0 Comments