HEADLINES

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA WANAHABARI

Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeahidi kushughulikia changamoto za Vyombo vya Habari na Waandishi wa Habari, ikiwemo Sera ya Habari na Utangazaji inayotaka Mwekezaji wa nje ya nchi kumiliki asilimia 49 na mzawa asilimia 51.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi ameelezea azma hiyo ya Serikali kufuatia hali halisi ya Uchumi wa Sekta ya Habari kushuka, pamoja na hali halisi ya maslahi ya Wanahabari hapa nchini.

Akiongea katika Mkutano wake wa kwanza na taasisi za habari nchini Disemba 18, 2024 katika ukumbi wa JNICC Jijini  Dar es Salaam, tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo, Prof. Kabudi amesema kuwa, changamoto nyingine zinazoikabili Sekta ya habari ni pamoja na kuyumba kwa uchumi wa Vyombo vya Habari na Waandishi wa habari kukosa mikataba ya ajira.

Prof. Kabudi ameendelea kusema kuwa, Sekta ya Habari ina changamoto kubwa ya mafao ya uzeeni, ambapo asilimia kubwa ya Wanahabari  wakistaafu kazi hiyo, wanakuwa na hali mbaya kiuchumi  pia  kukua kwa Teknolojia ya Mawasiliano kuliko sababisha hadhira kupungua kwenye Vyombo vya Habari vya asili.  

Profesa Kabudi ameeleza kuwa, Vyombo vya Habari vimeathiriwa kiuchumi ikiwemo kupungua kwa mapato kutoka kwenye matangazo na gharama kubwa za uendeshaji.

“Sera yetu ya Habari ya mwaka 2003 katika kifungu cha 3(2) inaelekeza kuwa wawekezaji katika Sekta ya Habari kutoka nje ya Tanzania wanapaswa wawe na ukomo wa asilimia 49, huku ikitoa nafasi kwa wawekezaji wa ndani kuwa na asilimia 51.

“Serikali inatambua changamoto hizi na tutaendelea kutafuta njia za kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha vyombo vya habari vinatoa huduma kwa ufanisi, na kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kumesababisha kuongezeka kwa ushindani wa hadhira kati ya vyombo vya habari vya asili na mitandao,” amesema Waziri Prof. Kabudi.

"Hii imetokana na tabia ya hadhira kupungua kutoka kwenye Radio, Televisheni na Magazeti na kutumia zaidi mitandao ya kijamii kwa sababu ya uharaka wa kupata habari, pia akili mnemba imeongeza mabadiliko hayo.” amesema.

Ametoa wito kwa Vyombo vya Habari kubadili mtazamo ili kukabiliana na mabadiliko ya Teknolojia ili yawe na mafanikio.



#KAZIINAONGEA



 

Post a Comment

0 Comments