HEADLINES

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YA DKT. SAMIA KUTATUA CHANGAMOTO YA MAKAZI WATUMISHI WA UMMA


Na Mwandishi Wetu,

Uhaba wa makazi kwa watumishi wa umma ni tatizo kubwa hapa nchini ambalo limekuwa likisababisha athari katika maisha yao ya kila siku.

Changamoto hii kwa watumishi wa umma, ni moja ya sababu zinazo sababisha kupungua kwa ufanisi kutokana na adha za umbali wa makazi na usafiri, hali inayochangia kuwaathiri  kiutendaji.

Ili kutatua tatizo la uhaba wa makazi kwa watumishi wa umma, Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo taasisi ya Watumishi Housing Investment (WHI) imezindua Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma ambao lengo lake ni kuhakikisha watumishi wa umma wa ngazi mbalimbali wanaishi katika makazi bora.

Kupitia mpango huo, jumla ya nyumba 1006 zimejengwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini lengo likiwa ni kujenga nyumba 5,000 kwa ajili ya watumishi wa umma.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa mpango huo  katika eneo la Njedengwa, Manispaa ya Dodoma Disemba 12, 2024 Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amesema tatizo la makazi kwa watumishi wa umma ni kubwa, hivyo mpango huo una lengo la kuwawezesha watumishi wa umma kuishi jirani na maeneo yao ya kazi.

Anasema ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa mpango huo, taasisi ya Watumishi Housing Investment ipo katika mazungumzo na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuangalia namna ambavyo itaweza kupata ardhi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo.

Waziri Simbachawene anaeleza kuwa, WHI haina ardhi hivyo inalazimika kununua ardhi kwa gharama kubwa jambo ambalo huongeza bei ya nyumba, lakini iwapo TAMISEMI itatoa ardhi nyumba zitaweza kujengwa jirani na maeneo ya kazi ya watumishi na kuwezesha nyumba hizo kuuzwa kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa WHI Dkt. Fred Msemwa anasema mpango huo unalenga kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba za watumishi, kuboresha miuundombinu katika maeneo ya makazi na kuweka mifumo bora ya utoaji wa mikopo kwa watumishi wanaotaka kujenga nyumba zao wenyewe.

Anasema, WHI inashirikiana na benki mbalimbali za hapa nchini kama CRDB, NMB, Azania, Exim ambazo zinatoa mikopo kwa watumishi kwa ajili ya kununua nyumba ambapo katika kipindi cha mwaka 2022/23 jumla ya shilingi bilioni 87 zimetumika katika utekelezaji wa mradi huo.

Akizindua mpango huo, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amwsema kuwa, ili mpango huo uweze kuwa na matokeo chanya, kuna haja ya kuwepo utaratibu ambao utakuwa rafiki utakaowawezesha watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii kununua nyumba kwa mishahara yao kwa kulipa kidogo kidogo.

Makamu wa Rais amesema
 mpango huo unalenga kupunguza tatizo la makazi kwa watumishi wa umma lakini pia ni kichocheo cha uchumi kwa utekelezaji wa miradi ya ujenzi na huchangia kutoa ajira.

Aidha Waziri Mpango ameongeza kuwa, serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaamini kuwa, nyumba zinazojengwa kupitia mpango huo zitatatua tatizo la makazi na kuchochea uwajibikaji kwa watumishi na kutoa huduma bora.

Dk. Mpango ameshauri kuwepo kwa uwazi na kuzingatiwa kwa vigezo na masharti na vifanyike kwa haki ambapo ameishauri ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa Umma na utawala bora, Wizara ya Ardhi na TAMISEMI kufanyia kazi suala la kupatikana kwa maeneo ya ujenzi wa nyumba jirani na maeneo ya kazi kwa watumishi wa umma.

Changamoto za makazi kimekuwa ni kilio cha watumishi walio wengi nchini, kuna sababu nyingi zinazochangia tatizo hilo ikiwemo ongezeko la idadi ya watumishi, kupanda kwa bei ya ardhi na vifaa vya ujenzi na kusababisha watumishi wengi kukabiliwa na ugumu wa kupata makazi bora kwa bei nafuu.

#KAZIINAONGEA

Post a Comment

0 Comments