Na Mwandishi Wetu,
DODOMA.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amesema Wizara kupitia vyombo vya usalama na taasisi nyingine za Serikali zitashirikiana na Vijana ili kupata suluhu kwa baadhi ya changamoto zilizopo na zinazoendelea kujitokeza katika jamii ikiwa ni pamoja uhalifu, kupambana rushwa, dawa za kulevya na Unyanyasaji wa kijinsia.
Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo Disemba 14, 2024, wakati akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Skauti Tanzania uliofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa Bungeni, jijini Dodoma.
"Tuna nia ya dhati kushirikiana na Vijana wa Skauti katika kushughulikia masuala ya kihalifu, nina amini kabisa kupitia jukwaa hili tutaweza kwenda kwa jamii kupitia mafunzo na utimamu mlio nao kuifanya nchi izidi kuwa bora ya amani na usalama” amesema Bashungwa.
Hata hivyo, Waziri Bashungwa amesisitiza umuhimu wa vijana wa skauti katika kutunza maadili ya Nchi na kuhamasisha vijana wengine kutokuingia kwenye vitendo vya uvunjaji wa sheria vinavyoharibu muelekeo wa maisha yao.
"kijana ukiingia kwenye dawa za kulevya unapoteza muelekeo na sisi hatufurahii kuona kijana anapoteza muelekeo na kuvunja sheria ya nchi kwahiyo tunajukumu kubwa la kuwasaidia" amesisitiza.
Aidha, Amesema Wizara kupitia Vyombo vyake vya Usalama ina programu mbalimbali ambazo vijana wakishirikishwa itasaidia jamii iwe salama pamoja na mali zao.
Nae, Rais wa Chama cha Skauti Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda amesema kazi kubwa ya skauti ni kukuza na kulinda maadili ya Mtanzania, kuendeleza ujasiri hasa kwa vijana kujishughulisha na shughuli za maendeleo kwa jamii.
Kwa Upande wake, Skauti Mkuu wa Tanzania, Rashid Kassim Mchata amesema dhumuni la Mkutano huu ni kupitisha rasimu ya mabadiliko ya Katiba ya chama ili kukidhi mahitaji ya sasa na kupitisha sera mbalimbali za chama.
0 Comments