Na Mwandishi Wetu,
RUFIJI.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipandisha hadhi Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji kuwa Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Mji wa Geita kuwa Manispaa.
Mchengerwa ameyasema hayo Disemba 13, 2024 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Rufiji kwenye uwanja wa ujamaa - Ikwiriri walifurika kushuhudia uzinduzi wa Tamasha la Bibi Titi Mohamed.
Amesema “Bibi Titi Mohamed huko aliko atakua anafurahia sana maendeleo ya Rufiji maana ndiye Mbunge wa kwanza aliyeasisi jimbo hili alifanya kazi kubwa sana na mimi Mbunge wa tisa naendeleza kazi aliyoianza Hayati Bibi Titi na pia Rais amefanya kazi kubwa kwa kuleta miradi mingi katika Wilaya yetu na sasa ameipandisha hadhi kuwa Halmashauri ya Mji.”
Amefafanua kuwa hadhi ya Mji ina maana kubwa sana kwa wananchi wa Rufiji kwa kuwa itakua miongoni mwa Halmashauri zinazonufaika na miradi mikubwa ya Benki ya Dunia na maendeleo yanakwenda kwa kasi katika kila Kata masoko yatajengwa, huduma za Afya zitapatika na miradi ya elimu itaongezeka.
“Tunamshkuru Rais kwa kuiona Rufiji na kuipa hadhi ya kuwa Mji na sasa maendeleo katika Wilaya hii katika nyanja zote yataenda kwa kasi zaidi,”amesema.
Tamasha la Bibi Titi linafanyika wilayani Rufiji kwa siku tatu kuanzia Disemba 12-14, 2024 kwa lengo la kumuenzi shujaa Bibi Titi Mohamed kama mwanamke wa kwanza kupigania uhuru na Mbunge kwa kwanza wa Rufiji.
#KAZIINAONGEA
0 Comments