HEADLINES

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA AWALILIA 15 WALIOKUFA KWA AJALI


Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa pole kwa familia za wananchi 15, waliopoteza maisha kwenye ajali iliyotokea usiku wa kuamkia leo Desemba 18,2024 mkoani Morogoro.

Katika ukurasa wake wa WhatsApp channel,  Rais Dkt. Samia ameandika kuwa: Usiku wa kuamkia leo Desemba 18 2024 tumepoteza ndugu zetu 15 kwa ajali ya barabarani, iliyohusisha lori la mizigo na gari la abiria aina Coaster katika eneo la Mikese, Barabara Kuu ya Morogoro - Dar es Salaam (A7 Highway).

Ninawapa pole familia, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima, ndugu, jamaa na marafiki. Ninawaombea kwa Mwenyezi Mungu ndugu zetu hawa wapumzike kwa amani, na majeruhi wote wapone kwa haraka.

Mbali na wito wangu kwa umma na maelekezo niliyolipa Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama Desemba 4 mwaka huu kuhusu kuongeza umakini na usimamizi katika Sheria za Usalama Barabarani, leo nimeliagiza Jeshi la Polisi kuwa na mfumo wa Leseni za Udereva utakaoweza kuwapunguzia alama (points) madereva wanaofanya makosa yenye kuhatarisha usalama na uhai barabarani. Mfumo huu uweke taarifa (records) kielektroniki za mwenendo wa makosa ya madereva barabarani kitakwimu, na kisha utumike kuamua kama wanastahili kuendelea kuwa na leseni za udereva au la. Hii ni katika kuboresha mfumo wa sasa ambao mara nyingi dereva hulipa faini pekee na kuachwa kuendelea kuwepo barabarani.

Uhai wa binadamu hauna mbadala, na hatuna budi kuendelea kuchukua hatua za pamoja na madhubuti kuhakikisha unalindwa kwa nguvu zote. Hatua hizi ni pamoja na kuhakikisha vyombo vya moto vinavyoingia barabarani vina sifa na vigezo vya kutumia barabara, na wale wanaoviendesha wana sifa, vigezo na rekodi za kustahili kuendelea kufanya hivyo.


#KAZIINAONGEA

Post a Comment

0 Comments