Na Lubango Mleka,
IGUNGA,
WAZAZI waliojifungua watoto kabla ya wakati wameshauriwa kuwa na subira wanapokuwa hospitalini kwa ajili ya kupatiwa huduma, kwani watoto hao hupitia changamoto nyingi ambazo wazazi ni vigumu kuzifahamu na kuzitatua kwa wakati.
Ushauri huo umetolewa na Rehema Iddi mkazi wa Wilaya ya Nzega mkoani Tabora,Novemba 20, 2024 katika hafla iliyohusisha madaktari, wauguzi na wazazi waliojifungua watoto kabla ya hospitali hapo.
"Napenda kuwashauri Wazazi wenzangu tunapokuwa wodini tusiwe na haraka ya kurudi nyumbani, haraka inaweza kusababisha athari kubwa kwa mtoto ikiwamo hata kifo" amesema Rehema.
Akitoa ushuhuda, alisema yeye alijifungua watoto mapacha mmoja alikuwa na uzito wa kilogram 1 na mwingine 1.1kg na amekaa wodini kwa siku 48 akisaidiana na wauguzi na madaktari katika kuwahudumia.
Mtoto mmoja Mungu alimchukua na niliye naye hadi natoka hospitalini alikuwa na uzito wa kilo 2, naishukuru Hospitali ya Rufaa ya Nkinga kwa huduma nzuri waliyonipatia kupitia wauguzi na manesi, sasa hivi mtoto wangu ana umri wa miezi 10 na uzito wa kilo 7, " amesema Rehema na kuongeza kuwa.
"Watoto hawa wanahitaji uangalifu sana, hawahitaji baridi na wala hawahitaji joto kali, mzazi ukiwa nyumbani inakuwa ngumu kutambua haya." amesema Rehema.
Naye Mkuu wa idara ya watoto (Paediatric) wa hospitali hiyo ambaye pia ni Daktari bingwa wa watoto, Jacqueline Suba amesema, licha ya watoto hao kukabiliwa na changamoto mbalimbali katika ukuaji wao, wanakabiliwa na changamoto ya kujisahau, kupumua katika kipindi cha sekunde 20, hivyo mama akiwa nyumbani ni vigumu kumhudumia kwakuwa atahitaji kukaa kwenye Oxygen.
Hafla hiyo imejiri katika kuadhimisha siku ya mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati inayofanyika Novemba 17 kila mwaka, ambapo Hospitali ya Rufaa ya Nkinga kupitia idara ya watoto imeona vema kuiadhimisha kwa kukumbushana mambo kadhaa na watendakazi wa idara zingine pamoja na wazazi waliojifungua watoto hao.
0 Comments