Na Mwandishi Wetu,
DAR ES SALAAM.
● Lengo ni kupunguza gharama za matibabu ya Kibingwa nje ya nchi
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea na utekelezaji wake wa mpango kuhakikisha inatoa huduma za Kibingwa bobezi nchini kwa ajili ya kuanza kutoa upandikizaji wa Ini ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025.
Hatua hiyo ya Serikali ni jitihada zinazoendelea kufanywa tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani miaka mitatu iliyopita.
Katika hatua hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Afya, imeanza utayarishaji kwa ajili ya kutoa huduma hiyo bobezi ya Kibingwa, ya Upandikizaji wa Ini, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Lengo la Serikali ni kusogeza huduma hizo karibu na wananchi ambazo hazikuwepo kutokana na Utaalamu, Vifaa vya uchunguzi au Miundombinu stahiki ya kutolea huduma hizo na hivyo kuigharimu Serikali fedha nyingi kupeleka wagonjwa hao kutibiwa nje ya nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi amefafanua kuwa, Hospitali imeingia makubaliano na Hospitali mbalimbali Duniani zenye ujuzi huo ili kuanza matayarisho kwa kushirikiana na wataalamu wazalendo kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025, Tanzania inaanza kutoa huduma hiyo.
Katika ufafanuzi wake, Prof. Janabi ameeleza kuwa, wiki hii Muhimbili imeshirikiana na wataalamu kutoka Hospitali ya Fortis ya nchini India ambao wamekua na Madaktari wetu ambapo kwa siku tatu wameona wagonjwa zaidi ya 100 wenye changamoto mbalimbali za magonjwa ya ini na kutathmini hali ya upatikanaji wa dawa, miundombinu ya maabara, ICU ambayo inakidhi mahitaji ya huduma hiyo.
Daktari Bingwa mbobezi wa upandikizaji ini Dkt. Gaurav Gupta kutoka Hospitali ya Fortis na Jenifer Choudhary, Mkurugenzi wa Biashara kutoka Vaidam Health wamesisitiza kuwa watatoa ushirikiano na utaalamu unaohitajika kuhakikisha Hospitali ya Muhimbili (MNH), inafikia lengo la uanzishwaji wa huduma hii hapa nchini.
#KAZIINAONGEA
0 Comments