Na Mwandishi Wetu,
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) unatekeleza mradi wa Shilingi Bilioni 19 wa kusambaza umeme katika vitongoji 180 utakaonufaisha Kaya 5,940 Mkoani Tabora.
Hayo yameelezwa na Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Magharibi, Robert Dulle Novemba 07, 2024 Mkoani Tabora mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Paul Chacha wakati wa kumtambulisha Mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo Kampuni ya Sinotec Company Ltd kutoka nchini China.
“Napenda kuwafahamisha wananchi wa Tabora kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dokta. Samia Suluhu Hassan ameridhia kiasi cha shilingi 19,057,015,682.55 kitumike kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 180 mkoani hapa na leo hii tuna mtambulisha mkandarasi anayetekeleza mradi huu,” alibainisha Mhandisi Dulle.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha alimuelekeza Mkandarasi kuhakikisha anakamalisha kazi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa na aliipongeza REA kwa kuendelea kutimiza dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo.
Akielezea utekelezaji wa mradi, Mhandisi Dulle amesema unatekelezwa ndani ya majimbo yote 12 ya mkoani humo na kwamba unatekelezwa kwa muda wa miaka miwili na utakamilika Mwezi Agosti, 2026 ambapo kila jimbo vitongoji 15 vitanufaika.
Amefafanua kuwa hadi sasa vitongoji vilivyosambaziwa umeme ni vitongoji 1,323 kati ya vitongoji 3,749 na kwamba vitongoji vitakavyosalia vitasambaziwa umeme kulingana na upatikanaji wa fedha.
“Vitongoji vitakavyonufaika ni kutoka katika Majimbo ya Sikonge, Urambo, Igalula, Tabora Kaskazini, Kaliua, Ulyankulu, Bukene, Nzega Vijijini, Nzega Mjini, Igunga, Tabora Mjini na Manonga ambapo kila jimbo litapata vitongoji 15, Mashine umba 15 na wateja 495 na msongo mdogo (LV) umbali wa kilomita 30,” amefafanua Mhandisi Dulle.
Naye Meneja wa Mradi kutoka Kampuni ya Sinotec Company Ltd, Mhandisi Alphred Kessy alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa watakamilisha mradi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
#KAZIINAONGEA
0 Comments