Na Mwandishi Wetu,
SONGWE.
Mazingira mazuri na wezeshi ya uwekezaji yaliyowekwa na serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yamesaidia Tanzania kuendelea kuongeza mitambo ya uchakataji na uchenjuaji wa dhahabu.
Novemba 17,2024 Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda amezindua kiwanda na mtambo wa kisasa wa uchakataji na uchenjuaji wa dhahabu unaotumia teknolojia ya Carbon-In-Pulp (CIP) wenye thamani ya zaidi ya Shilingi 10 bilioni unaomilikiwa na mwekezaji mzawa, Fredrick Ashery Meshack kupitia Kampuni ya Green Pacific Invistement Limited katika Kata ya Mbangala Wilayani Songwe.
Uzinduzi huo umefanyika katika eneo la mradi lililopo Kata ya Mbangala Wilaya ya Songwe na Itunda alimpongeza mwekezaji huyo mzawa kwa kuthubutu na kufanya uwekezaji mkubwa katika wilaya hiyo.
Itunda amesema kuwa, mwekezaji huyo amekuwa kijana mwenye mipango anayeziishi ndoto zake huku akitoa wito kwa vijana kujifunza kwake ili kupata wawekezaji wengine katika sekta ya madini wilayani humo.
Mkuu huyo wa Wilaya huyo amesema kuwa uwekezaji huo unatokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na Rais Dkt. Samia kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwekezaji huyo amesema kuwa anaishukuru Serikali na Benk ya NMB kwa kuwezesha mkopo wa zaidi ya Sh10 bilioni ambazo zimetumika kujenga mtambo huo.
Ametoa wito kwa wachimbaji na vijana kutokata tamaa akisema kuwa anaamini kuwa inawezekana kufikia malengo kama mtu atayasimamia, na kutaka vijana wasiogope.
Aidha amewataka wachimbaji kujenga mahusianbo mazuri na uaminifu kwa taasisi za fedha ili kuweza kutengeneza mazingira ya kukopesheka na kufanya uwekezaji.
Kuanzishwa kwa mtambo huo kutasaidia kuchangia mapato katika mfuko mkuu wa Serikali ya zaidi ya Shilingi bilioni 2 kwa mwaka na kuzalisha ajira zaidi ya 200 kwa wananchi wa Songwe na Tanzania kwa ujumla.
#KAZIINAO
NGEA
0 Comments