HEADLINES

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAENDELEA KUTIMIZA AHADI YA KUGAWA MAHINDI KWA WANANCHI WA NGORONGORO WALIOHAMIA MSOMERA


Na Mwandishi wetu,

 Msomera Handeni.

Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeendelea kutimiza ahadi ya kugawa chakula kwa wananchi waliotoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro na kuhamia kijiji cha msomera kwa kuwapa gunia 2 za mahindi kila kaya ambapo mpango huo hufanyika kila baada ya miezi mitatu kwa kipindi cha miezi 18 wakiwa wanaendelea kuzoea mazingira.

Akiongoza zoezi la ugawaji wa mahindi tarehe 18/09/2024, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa uhifadhi anayesimamia idara ya Maendeleo ya Jamii Gloria Bideberi, alisema kuwa zoezi la ugawaji wa mahindi kwa wananchi hao ni endelevu na linafanyika kila baada ya miezi mitatu kwa kadri wananchi wanavyoendelea kuhamia katika Kijiji cha Msomera. 

“Sisi kama Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro tunaendelea na utekelezaji wa maagizo ya Serikali kuhakikisha kuwa kila mwananchi wa Ngorongoro aliyehamia Msomera pamoja na nyumba na huduma nyingine ambazo anapewa na Serikali, tunahakikisha pia anapatiwa Mahindi jumla ya magunia 12 kwa  muda wa Miezi 18 ya mwanzo akiwa bado anajipanga kuandaa shamba alilopewa” alisema Kamishina Gloria 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Wakili Abert Msando ameeleza kuwa zoezi la ugawaji wa mahindi kwa wananchi hao ni mpango wa Serikali wa kuhakikisha kuwa wanachi wote wanaohamia Msomera wanapatiwa maisha bora zaidi tofauti na walikotoka ambapo sheria za uhifadhi zinawabana kufanya baadhi ya shughuli kama kilimo.

“Serikali inaendelea  kuhakikisha kuwa wananchi wanapofika Msomera wanapatiwa mahindi ili kuwawezesha kujipatia chakula wakati wakiwa wanajiandaa na  msimu wa kilimo kwenye eneo la ekari 2.5 lililopo kwenye nyumba aliyokabidhiwa na Serikalai na ekari zingine tano ambazo amepewa mahsusi kwa ajili ya kilimo cha mazao mbalimbali” Alisema  Msando 

Sabore Olemoko ambaye ni mmoja kati ya wananchi wanaonufaika na program hiyo ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali na kubainisha kuwa wanafurahia maisha wanayoishi Msomera hasa kukuta huduma zote muhimu za kijamii na fursa za kiuchumi ambazo serikali imewaahidi.

“Tunapenda kuishukuru Serikali yetu kwani baada ya kuhamia Msomera tumenufaika kwa vitu vingi kama vile mashamba, nyumba, zahanati, maji, shule, mabwawa, maeneo ya malisho, minada na leo tupo hapa tunapokea mahindi kwa ajili ya chakula cha familia zetu amnacho kinatusaidia kwa wakati huu ambao tunasubiri msimu wa kilimo uanze ili tuanze kulima mazao mbalimbali na kuanza kujitegemea kama wenzetu ambao walitangulia miaka miwili iliyopita” alisema Sabore.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaendelea na utekelezaji wa maagizo ya Serikali ambapo hadi kufikia tarehe 18 septemba, 2024  jumla ya kaya 1451 zimenufaika na mgao wa mahindi takribani tani 945 kwa awamu tofauti.

Post a Comment

0 Comments