HEADLINES

6/recent/ticker-posts

TAHARUKI YA WANYAMA WAKALI YAENDELEA KUWA TISHIO KWA WANANCHI WANAOISHI NDANI YA HIFADHI YA NGORONGORO.

Na Mwandishi Wetu,
NGORONGORO.

Wananchi wa tarafa ya Ngorongoro wilayani Ngorongoro wameendelea kuishi maisha magumu kutokana  na Kushambuliwa  na wanyama wakali kufuatia matukio yanayoendelea kutokea katika eneo hilo.

Afisa tarafa wa eneo hilo  bwana Bahati Mfungo amethibitisha  kutokea kwa matukio hayo na kusema kadri siku zinavyozidi kusonga  mbele hali imekuwa ni ya kutisha.

Katika  matukio ya hivi  karibuni  zaidi ya matukio mawili yameripotiwa kutokea  kwa wananchi na mifugo kupoteza maisha au kujeruhiwa vibaya katika tarafa hiyo.

Mwananchi  anayejulikana kwa jina la Orkendenye Liarite  mwenye umri wa miaka 32  kutoka kijiji cha Bulati akiwa  machungani  alishambuliwa na simba ambapo alijeruhiwa vibaya huku ng’ombe wake  wawili wakiuliwa na simba huyo.

Mwananchi huyo amejeruhiwa ubavu wa kulia na usoni na kulazimika kukimbizwa haraka katika kituo cha afya cha Nainokanoka  kwa ajili ya matibabu.

Katika tukio lingine  mwananchi anayeitwa Kimirei Kuya mwenye  umri wa miaka 26 alivamiwa na kiboko ndani  ya nyumba yake  ambapo katika hali isiyo ya kawaida alishambuliwa vibaya mwilini.

Tukio hilo limetokea katika kijiji cha Esere kata ya Alaitole  ambapo mwananchi huyo alivamiwa na mnyama  huyo  na kuuawa.

Kufuatia matukio haya serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) inaendelea kutoa elimu,kuhamasisha , kuandikisha, kuthaminisha na kuhamisha wananchi ambao wanataka kuhama kwa hiyari ili kunusuru maisha ya watu hao.


Post a Comment

0 Comments