HEADLINES

6/recent/ticker-posts

SERIKALI IMEIMARISHA NGUVU KAZI SEKTA YA AFYA

Na Mwandishi Wetu,
DAR ES SALAAM.

 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali imeimarisha nguvu kazi katika Sekta ya Afya kwa
kuongeza taasisi zinazotoa mafunzo ya Afya na upatikanaji wa fursa za elimu ya juu kwa kada hiyo.

Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa amesema hayo leo Julai 30, 2024 wakati akifungua rasmi Kongamano la majadiliano ya Kitaifa kuhusu masuala ya rasilimali watu katika Sekta ya Afya linalofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar Es Salaam. 
"Serikali imefanya upanuzi wa Taasisi za mafunzo ya Afya ikiwemo vyuo vya uuguzi, ukunga na utabibu ili kuongeza idadi ya wahitimu ambapo hivi sasa Nchi yetu ina Taasisi 182 zikiwemo Taasisi 137 zinazomilikiwa na Sekta binafsi." Amesema Mhe. Majaliwa
Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya Sita imehakikisha fursa za masomo ya elimu ya juu zinapatikana kwa kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa ikiwemo wanaosomea kozi za Afya ambao wamekuwa wakipewa kipaumbele wakati wote kwa kupewa mikopo ya asilimia 100. 

Katika kuendeleza rasilimali watu Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa amesema suala hilo limeendelea
kuwa kipaumbele cha Serikali kwa kuongeza bajeti ya Sekta ya Elimu kila Mwaka ili kufanikisha ujenzi wa rasilimali watu wenye ujuzi, stadi muhimu na wanaoweza kumudu mahitaji ya ndani na ushindani wa kimataifa.

Aidha, Mhe. Majaliwa amesema Serikali imeimarisha huduma za Afya ya msingi, huduma za Afya ngazi ya Wilaya na sasa inaimarisha huduma hizo kwenye ngazi za Halmashauri zote nchini ili kupunguza umbali kwa wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni. 
"Kuhusu ajira na upangaji wa watumishi wa kada za Afya, katika kipindi cha Miaka Mitatu ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan watumishi Elfu 30,000 wameajiriwa wakiwemo Madaktari na kupangiwa vituo vya kazi vikiwemo vya vijijini ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za Afya kwa wananchi." Amesema Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa.

 

Post a Comment

0 Comments