Na Mwandishi Wetu,
DAR ES SALAAM.
Watumishi wa Afya nchini wametakiwa kwenda kufanya kazi katika Halmashauri za pembezoni mwa nchi ili kupunguza uhaba wa wataalamu hao unaokadiriwa kuwa ni zaidi ya asilimia 50.
Upungufu huo unaovikabili vituo vya Afya, Zahanati na baadhi ya Hospitali za Halmashauri umechangia kudhoofisha hali ya utoaji wa hudumaza Afya.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Julai 29, 2024 wakati wa Kongamano la kumbukizi la Rais Mstaafu Mhe. Benjamini Mkapa lililofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar Es Salaam/
"Niwatoe hofu watumishi wa Afya kutoogopa kufanya kazi katika maeneo ya pembezoni mwa nchi kwa kuwa huduma zote muhimu za kijamii zinapatikana ikiwemo umeme, barabara, maji pamoja na shule." Amesema Waziri Ummy
Amesema, leo mkutano huo utajadili masuala ya rasilimali watu kwenye Sekta ya Afya ambao ni uzalishaji wa wataalamu wa Afya ndani ya nchi, ubora wa watumishi wa Afya kwa kuhakikisha watumishi wanasalia kwenye maeneo waliyopangiwa kuhudumia wananchi.
Waziri Ummy amesema Hayati Rais Benjamini Mkapa alikua ni muumini na kinara waliofanya kazi kubwa ya kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za Afya ikiwemo Sheria ya Bima ya Afya ya NHIF aliyoiasisi Mwaka 2,000.
Waziri Ummy amesema, hivi sasa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) umekua ndio chanzo kikuu cha mapato yanayotokana na huduma zinazotolewa kupitia mfuko huo.
Kongamano hilo linakutanisha wadau mbalimbali katika Sekta ya Afya ambapo watajadili masuala mbalimbali kuhusu Sekta ya Afya ambapo linatarajiwa kufunguliwa rasmi kesho Julai 30, 2024 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa
"Tunategemea kupata maoni na ushauri wa wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya ikiwemo Sekta binafsi katika kutengeneza mkakati wa Sita wa Taifa wa Sekta ya Afya Mwaka 2026/2031 ambao inaendana na kukamilisha kwa dira ya Taifa ya Mwaka 2050." Amesema Waziri Ummy
0 Comments