Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amekutana na ujumbe wa Wawakilishi 11 wa Bunge la Wawakilishi-Congress kutoka nchini Marekani katika walioanza ziara nchini Mei 28,2024 na kuhitimisha Mei 31,2024 lengo ikiwa ni kujifunza kuhusu Uhifadhi nchini Tanzania.
Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) Juni 1,2024 wakati wakijiandaa kuondoka nchini Waziri Kairuki amesema amekutana na kuzungumza na wawakilishi hao kuhusu masuala mbalimbali ya uhifadhi, urejeshaji wa nyara, kudhibiti ujangili na kushirikiana katika kuelimisha wananchi masuala ya uhifadhi na mipaka yao.
“Tumewashukuru kwa namna ambavyo wameendelea kutoa ushirikiano na kusaidiana nasi kupitia Shirika la la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) katika jitihada mbalimbali za kuhakikisha tunakuwa na uhifadhi imara endelevu, harakati mbalimbali za kudhibiti ujangili pamoja na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusiana na suala zima la uhifadhi na kujua mipaka yao” Waziri Kairuki amesisitiza.
Vilevile, Mhe. Kairuki ametoa rai kwa Wabunge hao kuona namna bora ya kuendelea kushirikiana na taasisi zao hasa katika shughuli za uhifadhi na wanyamapori ili kuweza kuhakikisha kwamba uhifadhi wa Tanzania unaendelea kukua kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
0 Comments