HEADLINES

6/recent/ticker-posts

ALIYEMTAPELI RIDHIWANI KIKWETE KUSOTA GEREZANI MIAKA 7


 Na Mwandishi Wetu,
DAR ES SALAAM.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu Innocent Chengula (23) kwenda jela miaka saba, baada ya kupatikana na makosa sita likiwamo la kujipatia Sh4 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti na Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete.


Chengula alijipatia fedha hizo, baada ya kujitambulisha kwa Ridhiwani kuwa yeye Dk Hassan Abbas, ambaye kwa sasa ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii.

Pia, Mahakama hiyo imemuamuru Chengula kumlipa Ridhiwani kiasi cha Sh4 milioni, anachodaiwa kumtapeli.

Mbali na adhabu hiyo, Mahakama hiyo pia imetaifisha simu moja ya mkononi pamoja na laini tatu za simu alizokuwa akitumia mshtakiwa huyo na kuwa mali ya Serikali.

Uamuzi huo umetolewa leo, Juni 5, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Yusto Ruboroga wakati kesi hiyo ya jinai namba 139/2022 ilipoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hukumu.

Chengula ambaye ni mkazi wa Kigogo Luhanga, alikuwa anakabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutuma ujumbe wa maandishi kwenda katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp akijitambulisha kwa Ridhiwani Kikwete na Wallece Karia kuwa yeye ni Dk Hassan Abbas, wakati akijua kuwa ni uongo.

Post a Comment

0 Comments