HEADLINES

6/recent/ticker-posts

TANZANIA YASISITIZA UMOJA WA MATAIFA KUWA HAINA WATU WA ASILI


 Na Mwandishi Wetu,

NEW YORK, MAREKANI

 Kikao cha 23 cha Jukwaa la kudumu la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Watu wa Asili (UNPFII) kimemalizika jijini New York mapema wiki hii nchini Marekani ambapo ujumbe wa Tanzania uliohudhuria kikao hicho umewasisitizia wajumbe walioshiriki mkutano huo kutoka maataaifa mbalimbali kuwa hakuna watu wa asili Tanzania. 

Katika kikao hicho jumbe wa Tanzania umeongozwa na Prof. Hamisi M. Malebo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wajumbe wengine kutoka NCAA, Wizara ya Maliasili na Utalii, UNESCO tawi la Tanzania, Wizara ya Mambo ya Nje na Ofisi ya Waziri Mkuu uliueleza mkutano huo kuwa, Serikali na watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanasimama katika mshikamano na Watu wa Asili duniani kote ambao ni wakazi wa mwanzo kabisa wa maeneo yao ya asili ikiwa ni pamoja na yale yaliyovamiwa na kutawaliwa na walowezi wa kutoka nchi na tamaduni zingine. 

Ujumbe huo uliukumbusha mkutano huo kuwa, Tanzania ilikuwa ni koloni la Wajerumani na baadaye la Waingereza lakini ilipata uhuru wake mwaka 1961 ambapo Watanzania wanaojumuisha zaidi ya makabila 120, waliishi katika eneo ambalo sasa linajulikana kama Tanzania kwa zaidi ya miaka 5,000 iliyopita na kujenga taifa moja lenye umoja na amani na kuhakikisha kuwa watu wake wanaishi kwa maelewano na bila ubaguzi. 

Vilevile ujumbe wa Tanzania ulibainisha kuwa, katika suala la Watu wa Asili kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania hakuna kundi mahususi la Watu wa Asili nchini. Mtanzania yeyote mwenye asili ya Kiafrika kisheria ni raia na ni Mtanzania na hakuna kabila lenye haki zaidi ya lingine. 

Watu wa Tanzania kutoka katika makabila zaidi ya 120 wameunganishwa na tamaduni, urithi wa pamoja, maadili na desturi pamoja na lugha ya Kiswahili inayoadhimishwa duniani kote.

Kadhalika, katika mkutano huo Ujumbe wa Tanzania ulifafanua kuwa, kwa kuzingatia haki ya kujitawala, Serikali ya Tanzania imesisitiza msimamo wake na imani thabiti katika Umoja wa Mataifa na kukemea juhudi zozote hasi zenye lengo la kuvuruga mafanikio yaliyofikiwa ya kujenga taifa la watu walio sawa na huru.

Katika andiko lililowasilishwa kwenye kikao hicho  Prof. Hamisi M. Malebo alisisitiza kwa kuweka mambo katika muktadha mahsusi kuwa Waamasai hawawezi kuchukuliwa kuwa ni Watu wa Asili katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kwani walifika Ngorongoro takriban miaka 200 iliyopita na kuwakuta Wahadzabe waliokaa hapo kwa zaidi ya miaka 3,000 iliyopita na Wadatoga waliokuwa hapo kwa zaidi ya miaka 400 kabla ya kuwasili kwao. 

Katika wasilisho lake Prof. Malebo amesisitiza kuwa Waamasai waliwashambulia na kuwafukuza Wahadzabe na Wadatoga kutoka katika ardhi waliyoishi kwa miaka zaidi ya 3,000 na 400, mtawalia. Waamasai baada ya kuwafukuza Wahadzabe na Wadatoga, walilikalia eneo hilo. 

Suala la kabila moja kuvamia na kuondosha kabila lingine katika eneo la asili si jambo geni nchini Tanzania, lilitokea pia kwa Wandendeule ambao walishambuliwa na kufukuzwa katika eneo lao na Wangoni walioingia Songea kutokea Afrika Kusini, vile vile Wamakua ambao nao walipigwa vita na kufukuzwa katika eneo lao huko Mtwara na Wayao na Wamakonde kutokea Msumbiji.

Prof. Malebo alisisitiza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haikubaliani na dhana ya Watu wa Asili kwa vile haitendi haki kwa muktadha wa hali ya makabila ya Tanzania kwa kuwa kila kabila lililotangulia nchini kabla ya ujio wa Waamasai kimsingi ni la asili zaidi na hivyo Watanzania wote wenye asili ya Kiafrika ni raia na ni Watanzania, Kwa hiyo, siyo sahihi kuchagua kabila moja kati ya makabila zaidi ya 120 ya Tanzania yenye sifa stahiki na kuliita moja kuwa ni la asili. 

Prof. Malebo alihitimisha kwa kusisitiza katika kikao cha Jukwaa la Watu wa Asili na kuwaomba kuuelewa msimamo wa Serikali ya Tanzania pia kuwa mfumo wa umiliki wa ardhi nchini katika nchi yetu hautambui ardhi za mababu au ardhi za kimila wala ardhi za makabila. Ardhi inamilikiwa na umma na imekabidhiwa kwa Rais kama mdhamini kwa niaba ya Watanzania wote. Mtu anapewa haki ya kumiliki ardhi kwa kufuata utaratibu wa kisheria na kwa muda maalum. 

Alisisitiza zaidi kuwa ni makosa kudai kwamba Waamasai au kabila lolote wanafukuzwa katika ardhi yao au ardhi ya mababu zao au ardhi ya kimila kwa vile jambo hilo halipo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wala katika sheria za nchi yetu na hakuna mwananchi yeyote aliyefukuzwa Loliondo wala Ngorongoro. 

Alilisisitiza Jukwaa hilo kutambua kwamba zoezi linalofanyika Loliondo ni kunusuru uhifadhi wakati kwa Ngorongoro ni kuboresha Maisha ya wananchi wa Jamii ya Wafugaji kuelimishwa, kujiandikisha na  kuhamia kwa hiari maeneo salama zaidi kwa manufaa yao, usalama wao na kujipatia maendeleo kama Watanzania wengine.

Post a Comment

0 Comments