HEADLINES

6/recent/ticker-posts

SIKU SITA MAADHIMISHO YA KITAIFA WIKI YA ELIMU, UJUZI NA UBUNIFU KUANZA MEI 25 JIJINI TANGA


Na Mwandishi Wetu,
DODOMA.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza kuanza kwa Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayotarajiwa kufanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlal na ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Bahari Beach Jijini Tanga, kuanzia tarehe 25 hadi 31 Mei, 2024.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mei 23, 2024 Jijini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa Maadhimisho hayo yanakutanisha Taasisi, Mashirika, Wadau wa Maendeleo, Asasi, Watunga Sera, Wabunifu/Wagunduzi, na Wadau wengine kutoka ndani na nje ya nchi, kwa ajili ya mijadala na kubadilishana uzoefu juu ya masuala ya elimu, ujuzi na ubunifu.

Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa Maadhimisho hayo pia yatatoa fursa kwa Watafiti na Wabunifu wachanga kukutana na wawekezaji wanaoweza kuchangia katika kuendeleza na kubiasharisha bunifu na teknolojia zao.

"Kauli mbiu ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu mwaka 2024 ni Elimu, Ujuzi na Ubunifu kwa Uchumi Shindani ambayo inachagiza maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Aidha, msukumo katika masuala ya ujuzi na ubunifu utaongeza chachu katika ujenzi wa uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu kama inavyosadifiwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo 2021/22 – 2025/26 na hata katika Dira la Maendeleo ya Taifa ya 2050 ambayo sasa inaendelea kuandaliwa" amesisitiza Kiongozi huyo.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa katika maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu kwa mwaka 2024 yatahusisha matukio maonesho ya bunifu, teknolojia na bidhaa nyingine; Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU); Mashindano ya ujuzi Skills Competition kwa wanafunzi wa Vyuo vya Ufundi na Ufundi Stadi; na mikutano na midahalo juu ya mada mbalimbali kuhusu elimu, ujuzi, sayansi na teknolojia.

Aidha, zitafanyika shughuli nyingine zinazohusu sekta ya elimu hususan utoaji wa elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 toleo la mwaka 2023; na mtaala ulioboreshwa. Aidha, utafanyika uhamasishaji kwa wanafunzi kujiunga na programu mbalimbali za vyuo vya elimu ya juu utafanyika wakati wa maadhimisho hayo.

Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa, Ujuzi na Ubunifu mwaka huu yatazinduliwa rasmi tarehe 27 Mei, na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb.) na yatahitimishwa tarehe 31 Mei, 2024 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.)

Post a Comment

0 Comments