Na Mwandishi Wetu,
DAR ES SALAAM.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amebainisha kuwa, ugonjwa wa Kisukari na Shinikizo la Juu la Damu (High Blood Pressure) ni kati ya magonjwa Kumi yanayowasumbua Watanzania ambapo amewataka wananchi kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwemo ulaji wa vyakula pamoja na kufanya mazoezi.
Waziri Ummy amesema hayo leo Mei 4, 2024 baada ya kufanya mazoezi yakiongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ikiwa ni Jumamosi ya kwanza baada ya kutoa tamko kuwa kila Jumamosi itakua siku ya mazoezi kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:00 asubuhi.
Amesema, kuanzia muda huo wa asubuhi barabara inayoanzia kwenye Taasisi ya Saratani Ocean Road kupitia daraja la Tanzanite itafungwa kwa maagizo ya Serikali ili kupisha watu wanaofanya mazoezi wafanye kwa uhuru.
“Shinikizo la Juu la Damu (High Blood Pressure) pamoja na Kisukari ni kati ya magonjwa 10 yanayowasumbua Watanzania, wajibu wetu kama Wizara ni kuhakikisha tunawakinga wananchi wasipate magonjwa, ndio maana tumeiomba Serikali kuu kupitia kwa Waziri Mkuu kufungwa kwa barabara hii ili kupisha mazoezi.” Amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy amemshukuru Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kwa kukubali ombi hilo na kuongoza mazoezi kwa siku ya kwanza baada ya kutoa tamko la kufungwa kwa barabara hiyo kuazia Taasisi ya Saratani Ocean Road kupitia Daraja la Tanzanite hadi katika viwanja vya Furaha.
Amesema, mazoezi yanasaidia sana kukinga magonjwa hususan Kisukari na Shinikizo la Juu la Damu kwa zaidi ya asilimia 50 hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kufanya mazoezi kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu wa mazoezi.\
“Mhe. Waziri Mkuu nikuahidi Wizara ya Afya itaendelea kuweka nguvu katika kuwakinga wananchi wako na magonjwa Yasiyoambukiza ikiwemo kuwahimiza kufanya mazoezi pamoja na kuzingatia mtindo bora wa maisha.” Amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy ametoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Albert Chalamila pamoja na Wakuu wa Wilaya akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Hassan Bomboko kwa kuweza kuwahamasisha wananchi ambao wamejitokeza kwa wingi kufanya mazoezi.
“Mkuu wa Mkoa nikuahidi, Wizara ya Afya tutaviunga mkono vikundi vyote vya mazoezi (jogging) vya Mkoa wa Dar Es Salaam, tukae pamoja ili tuone mambo gani tunaweza kuyafanya kwa kuboresha ufanyaji wa mazoezi kila siku ya Jumamosi kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:00 asubuhi.” Amesema Waziri Ummy
0 Comments