Na Mwandishi Wetu,
DAR ES SALAAM
Mtandao wa Wanawake watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (CWHRDs TZ) umeendesha mafunzo kwa wanawake watetezi wa haki za binadamu chini ya mradi wa “Mwanamke Mtetezi mstahimilivu kwa maendeleo ya jamii” unaoshughulika na masuala ya uchechemuzi (Advocacy) wa kuwa na mazingira salama ya utetezi wa haki za binadamu.
Mafunzo hayo yaliyoanza Aprili 4, 2024 yamehudhuriwa na wanawake watetezi wa haki za binadamu takribani 27 kutoka Tanzania bara na visiwani, mafunzo yaliyolenga kuwajengea uwezo wanawake hao kuelewa dhana ya uchechemuzi inauohusiana na mazingira salama ya utetezi wa haki za binadamu hapa nchini pamoja na kutoa huduma za kiusalama kwa wanawake watetezi hasa waliofikwa na hatari wakati wakitekeleza majukumu ya utetezi.
Mafunzo haya yanayotarajiwa kukamilika April 5, 2024 yamewapa fursa wanawake watetezi kukutana na kueleza changamoto mbali mbali ambazo wame kuwa wakikumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao na namna ya kukabiliana nazo.
“Pamoja na kuwa sisi ni watetezi wa haki za binadamu, bado tunapaswa kuangalia mienendo yetu hasa mienendo inayoweza kutuweka katika hatari kama ulevi kupindukia Kwani inaweza kutupelekea kutengeneza mianya ya watu wasiopenda kazi zetu kutufikia na kutudhuru Kwa urahisi” Hilda Stuart Dadu, Mratibu Kitaifa, CWHRDs TZ.
Mafunzo haya yamekuja kufuatia changamoto mbali mbali ambazo zimekuwa zikishuhudiwa kuwakumba watetezi wa haki za binadamu hasa watetezi wanawake ambao katika jamii nyingi wame kuwa wakitazamwa kama viumbe dhaifu na watu wa sio sahihi katika kazi za utetezi wa haki za Binadamu.
0 Comments