Na AMEDEUS SOMI,
DAR ES SALAAM.
Madalali na Wasambaza nyaraka za Mahakama wametakiwa kufanya kazi zao kwa kuzingatia kanuni, sheria na maadili ili kuepuka kuichafua taswira ya Mahakama wanapokuwa wanatekeleza amri za Mahakama, kwa kuwa wao ndio wanasimama kati ya mteja wanaemuhudumia na mtoa haki ambae ni Mahakama..
Wito huo umetolewa na Jaji wa Rufani ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo wakati akifungua mafunzo ya watu wenye nia ya kufanya kazi ya Udalali na Usambazaji wa Nyaraka za Mahakama zaidi ya 30 kutoka katika mikoa mbalimbali nchini leo tarehe 15/04/2024.
Ufunguzi wa mafunzo haya ya kundi la 12 ambayo yameratibiwa na kuendeshwa na IJA, umefanyika katika ukumbi wa Chipeta uliyomo ndani ya Maktaba ya Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (Law School of Tanzania), jijini Dar es Salaam.
NYINGINEZO
Katika hotuba yake, Mhe. Jaji Kihwelo amesema kuwa endapo Madalali na Wasambaza nyaraka za Mahakama hawatazingatia sheria, kanuni na maadili yanayoongoza kazi zao, basi itakayochafuka ni taswira ya Mahakama na wala sio wao.
“Nawasihi watekeleze amri za Mahakama kwa namna ambavyo sheria inavyowataka watekeleze ili kupunguza malalamiko kwa wananchi, pia kutenda haki na kuepuka kuichafua sura ya Mahakama, kwa sababu mwananchi wa kawaida anaitambua Mahakama, yeye hamjui huyu dalali anaetekeleza hukumu ya Mahakama,”
Aidha, Mhe. Jaji Kihwelo amesema kuwa mafunzo haya yamesaidia kuleta utaratibu mzuri wa kuwapata madalali na wasambaza nyaraka za Mahakama pamoja na utekelezaji wa kazi hizo, tofauti na zamani ambapo utaratibu haukuwa mzuri na ulisababisha malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.
Kwa upande wake mratibu wa mafunzo ambaye pia ni Mhadhiri wa IJA, Bi. Fatuma Mgomba amesema kuwa lengo la Mafunzo haya ni kuboresha eneo la utoaji haki kwa kuhakikisha Mahakama inakuwa na Madalali na Wasambaza nyaraka za Mahakama wenye maadili, uweledi, mbinu bora na nyenzo za kisasa za kufanyia kazi.
Mafunzo hayo yatafanyika kwa muda wa wiki mbili kuanzia tarehe 15 Aprili hadi 30 Aprili, 2024, ambapo Washiriki watafanya mitihani ya kupima umahiri wao na watakaofaulu watapatiwa vyeti vya umahiri vinavyowapa sifa ya kuomba kazi hiyo.
IJA inaendesha mafunzo haya kwa mujibu wa Kanuni ya 4 na ya 6 za Kanuni za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama Na.363 za mwaka 2017.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo haya akiwemo, Mkurugenzi msaidizi wa kampuni ya Udalali ya Master Auction company Ltd kutoka Kahama mkoani Shinyanga, Bi. Gendo Shimbi amebainisha kuwa Mafunzo haya yatamsaidia kutenda kazi zake kwa ufanisi na uweledi na hivyo kuepuka migogoro na wananchi wanapokuwa wanatekeleza hukumu za Mahakama.
Pia ameongeza: “Mafunzo haya ni fursa kwa kila mmoja wetu, ni soko kubwa kwa sasa, kwa hiyo ni njia nzuri kwa mtu kujiajiri na kujipatia kipato.”
Nae Bw.Dietrich Kateule ambae ni Mkurugenzi wa kampuni ya udalali ya African dream Auction Mart ya jijini Arusha ameelezea matarajio yake katika mafunzo hayo kuwa ni kujua sheria na kanuni zote zinazoongoza kazi hiyo ili kuhakikisha haki inatekelezwa vema kwa pande zote mbili, ya mteja wanaemuhudumia na mtoa haki ambae ni Mahakama.
Aidha, Mafunzo haya yanasaidia kukuza Biashara na Uwekezaji kwa vile wahitimu wakishajiriwa na Mahakama kama Madalali wanakuwa na sifa ya kufanya kazi na mabenki nchini kama Madalali na wakusanya madeni.
0 Comments