Na Mwandishi Wetu,
NGORONGORO
Baadhi ya wananchi wanaoishi katika Kijiji cha Endulen ndani ya Tarafa ya Ngorongoro wameipongeza serikali kwa uamuzi wa kuwahamisha kwa hiyari kutoka kijijini hapo kutokana na kusumbuliwa na changamoto ya Wanyama pori wakali.
Wakizungumza katika zoezi la uelimishaji, uhamasishaji na uandikishaji baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wamesema kuwa kasi ya ongezeko la wanyama wakali na waharibifu kama fisi, chui, Nyati, simba na tembo imewafanya washindwe kufanya shughuli zao za maendeleo na hivyo kuamua kuondoka kuelekea Msomera na maeneo mengine.
Wamesema hawaoni sababu ya kuendelea kuishi katika eneo hilo wakati kuna maeneo mengi nchini ikiwemo Kijiji cha Msomera ambayo yametengwa na Serikali na watu wanaishi kwa amani bila kusumbuliwa na wanyama wakali wanaokula mifugo yao ndani ya hifadhi.
“Humu ndani ya hifadhi hatuna amani yoyote hasa kutokana na kukimbizana na wanyama wakali, maisha ya humu ndani ya hifadhi yamepitwa na wakati ndio maana nimeamua kujiandikisha kwa hiyari na kuondoka kwenda katika Kijiji cha Msomera,”alisema Bi Maria Lepilal mkazi wa kijiji cha Endulen.
Wakazi wengine wa Kijiji cha Naiyobi ambao majina yao tunayahifadhi kutokana na sababu za usalama wao wamesema kadri wanavyokubali kuhama kwa hiyari wamekuwa wakipokea vitisho na hata kutengwa kutoka kwa baadhi ya wanaharakati wanaotaka zoezi hlo likwame kwa maslahi yao wenyewe bila kujali hali ya wananchi.
“Wanaharakati na baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitushawishi kubaki humu ndani ili waendelee kututumia kwa sababu zao za kiuchumi bila kujali shida tunazopata, mwezi uliopita boma la jirani yangu kundi la fisi waliingia wakalaa mbuzi 7, ndiyo maana tunaamua tukijiandikisha tuondoke ili tukaanze maisha mapya na kuepukana na adha ya kuishi ndani ya hifadhi kama wanyamapori,”alisema mkazi mmoja wa Kijiji hicho.
Vijiji vya Naiyobi, nainokanoka, Kapenjiro, Osinoni, Olpiro, Meshili na Esere ni miongoni mwa vijiji vilivyopo katika tarafa ya Ngorongoro ambavyo vimepokea zoezi la kuhama kwa hiyari kwa ari kubwa ambapo baadhi ya wanaharakati wanaotaka zoezi hilo likwame wameamua kuondoka na kuhamia maeneo mengine.
0 Comments