HEADLINES

6/recent/ticker-posts

BILIONI 9.88 KUJENGA LAMI BARABARA YA DAREDA MJINI - DAREDA MISSION BABATI


 Na Mwandishi Wetu,

BABATI

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu Wakala wa Barabara (TANROADS) kumsimamia Mkandarasi kampuni ya Jiangxi Geo Engineering kukamilisha kwa wakati ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Dareda hadi Dongobesh (km 60) sehemu ya kwanza ya Dareda Mjini hadi Dareda Missioni (km 7) ili kuufungua kiuchumi Mkoa wa Manyara.

Bashungwa amezungumza hayo Wilayani Babati Mkoani Manyara Aprili 06, 2024 wakati akishuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo kati ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) na kampuni ya M/s Jiangxi Geo Engineering (Group) Corporation ya China kwa gharama ya Shilingi Billioni 9.88. 

“Tumempa Mkandarasi huyu kwa kuwa tayari anatekeleza miradi mingine ya barabara maeneo haya na jirani na tumemuongezea hii nyingine kwa kuwa si kilometa nyingi hivyo Mtendaji Mkuu sitaki kusikia visingizio nataka barabara hiyo ikamilike haraka maana hata Wakandarasi wa ndani kilometa saba wangeweza kuzijenga”, amesisitiza Bashungwa.

 Bashungwa amemtaka Mkandarasi huyo kuhakikisha anakamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Labay-Haydom (km25) na barabara ya Mbulu-Garbabi (km 25) ambapo Serikali inakwenda kulipa madeni ambayo alikuwa anayadai ili miradi yote iweze kukamilishwa kwa haraka.

Aidha, Bashungwa amempongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS kwa kutekeleza maagizo ya Wizara ya kutolimbikiza kazi nyingi kwa Mkandarasi mmoja na hivyo miradi mingi kuchelewa na kusababishia hasara Serikali.

“Nikupongeze Mtendaji Mkuu kwa kutumia hatua za kimkataba kumuondoa Mkandarasi wa barabara ya Lukuyufusi - Mkenda Mkoani Ruvuma mara baada ya kuona hafanyi vizuri kwenye maeneo mengine”, amesema Bashungwa.

Bashungwa amempongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS kwa kusimamia ushiriki wa Wahandisi Washauri wa ndani katika usimamizi wa miradi ambapo katika mradi huu usimamizi utatekelezwa kupitia Kitengo cha Usimamizi wa Miradi cha TANROADS (TECU).

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendinga amesema mradi huu unapita katika Wilaya ya Mbulu na Babati na ujenzi wa barabara hii inakwenda kuongeza thamani ya mazao ya shamba ikiwemo kilimo na ufugaji pia itarahisisha wananchi kufanya biashara pembezoni mwa barabara na kukuza uchumi wa mkulima mmoja mmoja na Mkoa kwa ujumla.

Vilevile, Sendinga ameomba Bajeti ya kimkakati kwa ajili ya matengenezo ya barabara kwa ajili ya Mkoa wa Manyara kutokana na Mkoa huo kuwa na mvua kubwa za mara kwa mara na kuleta athari kubwa ya miundombinu ya barabara.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo ameeleza kuwa wananchi wa Babati wamekuwa wakisubiria barabara hiyo kwa hamu sana ambapo ikikamilika itasaidia kukuza uchumi wa wana Babati na Mkoa wa Manyara kutokana na uzalishaji mkubwa wa kilimo unaofanyika.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta amesema Mkandarasi aliyeshinda zabuni ni kampuni ya M/s Jiangxi Geo Engineering (Group) Corporation ya China, kwa gharama ya Shilingi Billioni 9.88 ambapo utasimamiwa na Wataalamu wa ndani katika kitengo cha Usimamizi (TECU). 

Besta ameongeza kuwa zabuni kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya pili ya Dareda Mission – Dongobesh (Km 53) inatarajiwa kutangazwa katika Mwaka huu wa fedha 2023/24.

Post a Comment

0 Comments