Na Mwandishi Wetu,
DAR ES SALAAM.
Mchango kutoka kwa wadau wa mfuko wa Afya wa pamoja ikiwemo nchi ya Uswisi, Denmark, Ireland, Korea Kusini, UNFPA, UNICEF, pamoja na Benki ya Dunia kupitia awamu ya ufadhili wa moja kwa moja wa Kituo cha Afya (DHFF), (2021-2025) wamechangia kiasi cha Tshs: Bilioni 37.7 ili kusaidia kutokomeza Malaria nchini ifikapo mwaka 2030.
Waziri Ummy amesema hayo wakati wa kikao na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania Mhe. Didier Chassot kilichofanyika leo Aprili 8, 2024 katika ofisi za Wizara ya Afya Mkoani Dodoma ambapo kwa pamoja wamejadiliana masuala mbalimbali yenye manufaa kwa pande zote Mbili katika ushirikiano unaoendelea.
“Kwa niaba ya Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunashukuru kupitia kwako Mhe. Balozi kwa msaada wa Serikali ya Uswisi na ahadi zako ambazo umezitoa katika kusaidia Sekta ya Afya kupitia michango mbalimbali ya ruzuku.” Ametoa shukran hizo Waziri Ummy
Amesema, lengo la jumla la mradi ni kuchangia kutokomeza Malaria ifikapo mwaka 2030 kupitia ushirikishwaji wa wadau wa Kitaifa, baina ya kisekta na kikanda kwa kushawishi mijadala ya sera za Kimataifa na miongozo ya kiufundi kwa kushirikishana desturi za Kitanzania.
“Mradi huu unawanufaisha Watanzania (Bara na Zanzibar) wanaokabiliwa na changamoto kubwa ya ugonjwa wa Malaria hasa wale wa vijijini na wale walio katika makundi hatarishi zaidi (wajawazito na watoto, watu binafsi wanaoishi katika mazingira hatarishi)”. Amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy ameiomba Serikali ya Uswizi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutokomeza magonjwa ya ngono ikiwa ni pamoja na VVU, mimba zisizotarajiwa, ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia pamoja na kusaidia wahudumu wa Afya ngazi ya jamii (CHWs) ambao wana jukumu katika kutoa huduma muhimu za Afya kwa Jamii.
Kwa upande wake, Balozi wa Uswizi nchini Tanzania Mhe. Didier Chassot amesema Serikali ya Uswizi itaendelea na dhamira yake ya kuisaidia Sekta ya Afya nchini Tanzania ili kudumusha umoja uliopo baina ya nchi hizo Mbili.
“Serikali ya Uswizi itachangia kwa pamoja na Serikali ya Ujerumani kwa lengo la kuendeleza umoja wetu kwa kutoa msaada wa kiufundi kwa njia ya kujenga uwezo kwa taasisi zilizopewa mamlaka na uidhinishaji wa Bima ya Afya kwa Wote (UHI).” Amesema Balozi Chassot
0 Comments