Na Amedeus Somi,
DAR ES SALAAM.
Kamati ya Usimamizi na
Uendeshaji wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania leo imetangaza adhabu kwa
Wachezaji na Timu mbalimbali za Ligi Kuu ambapo Wachezaji wa Simba SC Kibu Denis
na Mzamiru Yassin wamepigwa faini ya Tsh milioni 1 kila mmoja kutokana na
kufanya vitendo vilivyoashiria imani za kishirikina.
“Kwenye mechi ya Coastal
Union FC 1-2 Simba SC, Wachezaji Kibu Denis na Mzamiru Yassin wa klabu ya Simba
wametozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kila mmoja kwa kosa la
kuonekana wakiondoa taulo la mlinda mlango wa klabu ya Coastal Union, Ley
Matampi lililokuwa limewekwa pembeni ya lango wakati mchezo”
“Jambo hilo liliashiria imani za kishirikina,
adhabu hii ni kwa kuzingatia Kanuni ya 41:5 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa
Wachezaji”
Wanalambalamba Azam Fc nao wamepigwa Faini ya
Shilingi Millioni 1. kwa kosa la wachezaji wake kuchelewa kuingia Uwanjani
katika mchezo wao dhidi Tabora United 0-0 katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi
Adhabu hii ni kwa kuzingatia Kanuni ya 17:33 na 17:60 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.
Klabu ya Azam Fc inatarajia kushuka dimbani Machi 17 katika mchezo wa Dar es Salaam Derby dhidi ya Vinara na Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Nbc Klabu ya Young Africans mchezo unaotarajia kupigwa katika nyasi za Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
0 Comments