Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza kuvunjwa kwa Bodi ya Kampuni Tanzu ya TANESCO ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO) na kuundwa upya kwa Menejimenti ya Kampuni hiyo kutokana na utendaji kazi mbovu, wizi fedha za umma ndani ya Shirika pamoja na wizi wa vifaa vya umeme uliokithiri.
Dkt. Biteko ametoa agizo hilo wakati wa Kikao kazi baina yake na Uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni zake tanzu, Wakurugenzi wa TANESCO wa Kanda na Mameneja wa Mikoa ambacho kimefanyika tarehe 28 Machi, 2024 jijini Mwanza kikiwa na lengo la kujadili utendaji kazi katika Sekta ya umeme.
Hatua hii inakuja ikiwa ni siku moja baada ya Bodi ya TANESCO kuagizwa kumuondoa Meneja Mkuu wa ETDCO kutokana na utendaji mbovu wa kazi ndani ya Taasisi na kusuasua kwa utekelezaji wa miradi ya umeme ukiwemo wa usafirishaji umeme kutoka Tabora hadi Urambo na Tabora hadi Mpanda.
Maamuzi hayo ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, yametokana baadhi ya watendaji wa TANESCO na kampuni zake Tanzu kushindwa kutekeleza maelekezo yake aliyoyatoa tarehe 2 Desemba 2023 ya kupambana na rushwa, kujenga mahusiano na wananchi wanaowahudumia, kuimarisha uaminifu ndani na nje ya Taasisi, kuacha visingizio na kutatua matatizo ya umeme yanaapojitokeza.
Dkt. Biteko ameagiza Watumishi wote wanaojihusisha na wizi ndani ya Shirika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria ikiwemo kuwaweka pembeni katika Utumishi maana wao ni sababu ya watanzania kutokupata umeme wa uhakika.
Aidha ameelekeza wananchi waliotoa taarifa zilizopelekea kubaini wezi hao wa vifaa vya umeme kupewa barua za pongezi na fedha taslimu.
Dkt. Biteko amewataja baadhi ya watumishi wasio waaminifu wa TANESCO ambao wamekuwa wakishiriki kufanya wizi wa vifaa mbalimbali ikiwemo vyenye asili ya shaba, mafuta ya transfoma, vifaa vya miradi na ujenzi wa laini haramu ambazo hazipo kwenye mipango ya TANESCO huku mtumishi akiwa amelipwa pesa binafsi.
Vilevile, Dkt. Biteko ametoa onyo kwa viwanda na wanaofanya biashara ya vyuma chakavu nchini, kuwa wakikutwa na vifaa vya umeme watachukuliwa hatua kali za kisheria na watu hao watachukuliwa kama wezi na si wanunuaji wa vifaa hivyo.
Ili kuimarisha utendaji wa TANESCO, Dkt. Biteko amesema kuwa kuanzia sasa kutakuwa na upimaji wa kazi mkoa kwa mkoa katika kila kipindi cha robo mwaka ambapo vigezo mbalimbali vitapimwa ikiwemo uhudumiaji wa wateja na kukatika mara kwa mara kwa umeme ambako muda mwingine kunatokana na uzembe wa kutochukua hatua kwa wakati.
Ameongeza kuwa, wale watakaoonekana hawana utendaji mzuri wa kazi watatafutiwa kazi nyingine.
Aidha, ameagiza Wakurugenzi na Mameneja wa Mikoa wa TANESCO kushirikiana na Wakuu wa Mikoa yote nchini katika kuimarisha ulinzi wa miundombinu ya umeme hasa katika kipindi hiki ambacho hali ya umeme inaendelea kuimarika na miundombinu hiyo ikihitajika kufikisha umeme kwa wananchi.
Dkt. Biteko pia ameagiza Kitengo cha Usalama ndani ya TANESCO kuendelea kuimarisha ulinzi wa vifaa vya umeme na kutofanya urafiki na wezi wa vifaa vya umeme.
Katika hatua nyingine Dkt. Biteko amesema kuwa kwa ujumla kazi nzuri inafanyika TANESCO akitolea mfano ufanyaji kazi wakati wa dharura umeimarika ikiwemo kurekebisha hitilafu mbalimbali zinapojitokeza.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amewataka watendaji wa TANESCO kujirekebisha wao wenyewe na wasisubiri kurekebishwa kwani yapo maeneo ambayo wanaweza kusimamia bila kusubiri viongozi ikiwemo kuwafanya watumishi walio chini kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi.
Amesema kuwa, maelezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati atayasimamia ipasavyo.
Pia Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio ameweka msisitizo kwa Watendaji wa TANESCO kuwa lazima wabadilishe taswira ya Shirika hilo kwa wananchi kwa kuhakikisha kuwa wanatoa huduma bora.
Baadhi ya Watendaji wa TANESCO kwenye kikao hicho wamekiri kuwa taswira ya Shirika hilo kwa wananchi bado inahitaji kuboreshwa ili kuweza kuaminika zaidi kwa wananchi ikiwemo taarifa mbalimbali zinazotolewa na Shirika hilo.
0 Comments