Na Mwandishi Wetu,
MAFIA.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Lazaro Kilahala kuhakikishia anasimamia masuala ya usalama katika vivuko vyote nchini ili viweze kutoa huduma bora pamoja na kulinda usalama wa mali na abiria.
Aidha, Bashungwa ametoa wiki moja kwa TEMESA kuhakikisha wanapeleka vichanja vya kuhifadhia shehena za mizigo na bidhaa katika Kivuko cha MV Kilindoni kinachotoa huduma za usafiri Wilayani Mafia na Nyamisati Mkoani Pwani.
Bashungwa ametoa maagizo hayo Machi 22, 2024 akiwa Wilayani Mafia wakati alipokagua utendaji wa Kivuko hicho na kusikiliza kero za wananchi wanaokitumia ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza Watendaji na Wakuu wa Taasisi za Serikali kuhakikisha wanatatua changamoto za wananchi kwa wakati kama maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyoelekeza.
“Nitoe maelekezo kwa TEMESA ndani ya wiki moja wawe wamefika hapa na kuleta vifaa vyote vinavyohitajika eneo la mizigo na vipangwe kwa mujibu wa taratibu kwani ni hatari, abiria ana mizigo kusafiri sehemu moja”, amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa ameitaka TEMESA kuhakikisha wanakisimamia Kivuko cha MV Kilindoni ambacho kina uwezo wa kuhudumia abiria 200 na magari 10 ili kiweze kutoa huduma bora na salama kwa wananchi wa Wilaya ya Mafia na Pwani kwa ujumla.
Naye, Mkazi wa Wilaya ya Mafia Bw. Mohamed Mswala ameishukuru Serikali kwa kupeleka kivuko hicho ambacho kimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Wilaya hiyo na kusema changamoto iliyopo ni kutokuwepo kwa vifaa vya kutosha vya kuhifadhia shehena za mizigo (maturubai na pallet) na kulazimu kupanga mizigo na bidhaa katika maeneo ya kukaa kwa abiria hasa katika vipindi vya mvua.
“Tunashukuru Serikali kwa kivuko hichi lakini tunaiomba Serikali itusaidie kupata vifaa vya kuhifadhia mizigo yetu kwani kuna muda mwingine tunapata kesi ya kulipa mizigo ya watu ambayo tumewasafirishia”, amesema Bw. Mohamed.
0 Comments