HEADLINES

6/recent/ticker-posts

WATUMISHI MOI WASHAURIWA KULIPWA KWA MATOKEO SIO ZIADA YA MUDA

Na Mwandishi Wetu,
DAR ES SALAAM.

Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Prof. Abel Makubi ameshauri kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa ulipaji posho za ziada kwa watumishi kwa kutumia kigezo cha matokeo za ziada (extra performance) baada ya kufikia lengo badala ya mfumo wa sasa wa muda wa ziada (extra duty) ili kuongeza ufanisi kazini.

Akifungua kikao cha Nne cha baraza la Tano la wafanyakazi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) katika ukumbi wa mikutano wa APC Bunju jijini Dar es Salaam Prof. Makubi amesema ni vema kuangalia upya kigezo hicho ili  kuongeza ufanisi na tija kazini.

“Tuhame kutoka kwenye mfumo wa kulipana muda wa ziada (extra duty) hadi kufikia utendaji wa ziada (extra performance), hatuwezi kuendesha taasisi kwa mfumo wa ‘extra duty’, unatakiwa ulipwe kwa utendaji wa ziada, kwahiyo tuende kwa mfumo huo wa ‘extra performance’.  amesema Prof. Abel Makubi 

Alifafanua kuwa “Mtumishi anaweza kuja kazini saa 12 asubuhi hadi saa mbili usiku na ukamlipa muda wa ziada, lakini ukija kuangalia ndani ya muda huo amefanya nini? …tunataka mtu afanye kazi ya ziada ili alipwe ni sawa lakini pia tuangalie ndani ya muda huo amehudumia wagonjwa wangapi ?

Amebainisha kuwa kipaumbele cha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni huduma bora, wizara ya afya nayo huduma bora, hivyo amewataka watumishi kutimiza wajibu wao wa kutoa huduma bora  kwanza na kuhakikisha  bidhaa za huduma zipo , na ndipo pia motisha zetu tuendelee kuboresha.  

“Kikao kitatuwezesha kutujulisha wapi tulikotoka na wapi tulipo na tunakokwenda, kikubwa kutatua changamoto ili kuboresha huduma, wananchi wanatutegemea na eneo kubwa wanaolotegemea wananchi ni utoaji wa huduma” amefafanua Prof. Makubi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa MOI

“Nawashukuru wafanyakazi wote wa MOI kwa kuboresha huduma hadi kufikia kiwango cha wananchi kutusifia, sio kwamba huduma zilikuwa sio nzuri, lakini wananchi wanapenda kuona huduma zinakuwa bora zaidi”

Akizungumzia changamoto za taasisi hiyo “Moja ya changamoto ni kuchelewa kwa huduma, baadhi ya wananchi wanalalamika, hili ni suala ambalo hatuwezi kuliondoa mara moja kwasababu linahusisha mazingira ya mgonjwa husika, hata hivyo tunaendelea kulipatia ufumbuzi, tujitahidi tusiwe sehemu ya kikwazo cha mgonjwa kupata huduma kwa wakati” 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wa afya serikalini (TUGHE) tawi la MOI Privatus Masula ameshauri maboresho ya huduma kwa wateja yasiwaache nyuma watumishi ili kuongeza hari ya kufanya kazi na kuomba masilahi ya wafanyakazi yatazwe zaidi na kuboreshwa.  

Mkiti huyo wa TUGHE ameahidi kuwa pamoja na Menejimenti katika kutekeleza falsafa ya ubora wa huduma na kila mtumishi kuwajibika kwa matokeo(performance).

Post a Comment

0 Comments