HEADLINES

6/recent/ticker-posts

TANZANIA YAJADILI NAMNA YA UNUNUZI WA DAWA ADIMU KUTOKA CUBA

Na Mwandishi Wetu,
DODOMA.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akiwa na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Grace Magembe pamoja na Wakurugenzi wa Wizara ya Afya leo Februari 2, 2024 wmekutana na Balozi wa Tanzania nchini Cuba Bw. Humphrey Polepole, wadau wa Hospitali, MSD pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) ambapo wamefanya mazungumzo katika ofisi za Wizara ya Afya Mkoani Dodoma.

Mazungumzo hayo yamelenga kuona namna gani Serikali ya Tanzania inaweza kuanzisha ushirikiano wa ununuzi wa dawa adimu moja kwa moja kutoka katika viwanda vya dawa vya nchini Cuba.

Balozi Polepole amesema hivi sasa Tanzania na ukanda wa nchi za SADC kuna uhaba wa dawa za kutibu magonjwa kama vidonda vitokanavyo na Kisukari, baridi yabisi pamoja na dawa za kutibu ugonjwa wa Vitirigo.


“Dawa hizi zinazalishwa nchini Cuba na kiwanda cha Biocube Pharma ambazo zimeonesha matokeo makubwa, hivi sasa wagonjwa wa Kisukari wenye vidonda ambavyo haviponi, nchini Cuba hawakatwi tena viungo kutokana na madhara yanayosababishwa na vidonda hivyo bali hutumia dawa hizo na kupona kabisa.” Amesema Bw. Polepole

Aidha, Balozi Polepole ameongeza kuwa kiwanda hicho kinazalisha dawa za kutibu ugonjwa wa vitirigo (mabaka meupe katika mwili) pamoja na baridi yabisi na imeonekana kuna uhitaji mkubwa wa dawa hizo nchini na ukanda wa nchi za SADC kwani kuna wananchi wengi wanasumbuliwa na maradhi hayo. 

Kwa upande wake, Waziri Ummy amemshukuru Balozi Polepole kwa weledi wake wa utendaji akiwa kama Balozi nchini Cuba kwa kutafuta fursa ambazo zitaisaidia Serikali kupunguza gharama za matibabu kwa watu wenye matatizo hayo.


“Sasa hivi Serikali inatumia gharama kubwa kwa matibabu ya watu wenye vidonda vitokanavyo na Kisukari, Baridi Yabisi pamoja na Vitirigo ambapo takwimu zinaonesha Hospitali ya Taifa Muhimbili pekee imetumia Shilingi bilioni 1.4 katika matibabu.” Amesema Waziri Ummy 
Waziri Ummy amemhakikishia Balozi Polepole kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya itaanza mchakato mara moja wa kununua dawa hizo ili ziwe mkombozi kwa watu wenye matatizo hayo hasa vidonda vitokanavyo na Kisukari ambavyo haviponi na wengi wao huishia kukatwa viungo.



Post a Comment

0 Comments