HEADLINES

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YATENGA ZAIDI YA BILIONI 899 KUAJIRI WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII

Na Mwandishi Wetu,
DAR ES SALAAM.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga jumla ya Tsh. bilioni 899.4 kwa ajili ya kutekeleza mpango wa kuajiri na kuwajengea uwezo jumla ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wapatao 137,294 katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdori Mpango jana Januari 31, 2024 kwenye Uzinduzi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii uliofanyika katika kituo cha Mkutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar Es Salaam.


“Utekelezaji wa Mpango huo utafanyika katika kipindi cha Miaka Mitano kwa awamu ambapo mwaka wa kwanza 2023-2024 zaidi ya wahudumu elfu 28,000 watafikiwa na baadaye wastani wa wahudumu elfu 27,324 kila mwaka kwa kipindi cha miaka Minne mfululizo kuanzia mwaka 2024-2025 hadi 2027-2028.” Amesema Makamu wa Rais Dkt. Mpango.

Aidha, Dkt. Mpango amezielekeza Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Mamlaka nyingine zinazohusika kwa kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi madhubuti wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ili uweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Dkt. Mpango amewasihi viongozi wote wanaohusika katika ngazi zote kuhakikisha zoezi la kuwachagua wahudumu hao wa Afya ngazi ya jamii linafanyika kwa kufuata vigezo na taratibu zilizowekwa ili kupata wahudumu wenye sifa stahiki watakaotekeleza majukumu hayo na kuwataka watakaopewa jukumu la kutekeleza mpango huo, kujiepusha na vitendo vya upendeleo, rushwa au ukiukwaji wa taratibu.


“Wahudumu wa Afya mtakaopewa dhamana ya kutekeleza jukumu hili zingatieni weledi na kujituma pamoja na kutoa rai kwa jamii kuupokea mpango huo na kuthamini huduma za wahudumu wa aAya ngazi ya Jamii kwa kuwapa ushirikiano wa kutosha ili kulinda na kuboresha Afya katika jamii.” Amesisitiza Makamu wa Rais Dkt. Mpango.

Post a Comment

0 Comments