HEADLINES

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA ANAMWAGA FEDHA KUTATUA KERO SEKTA ZA ELIMU, AFYA NA MIUNDOMBINU

Na Mwandishi Wetu,
TANGA,

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutoa fedha nyingi katika kutatua kero za Watanzania ikiwemo wananchi wa Mkoa wa Tanga na katika Sekta ya Maji ambapo ametoa Billioni 25 kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama katika Jiji la Tanga na maeneo ya pembezoni. 

Hayo yamesemwa leo Februari 22, 2024 na Waziri wa Afya na Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Mhe. Ummy Mwalimu kwenye ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Isdor Mpango wakati akizindua hati fungani ya kijani ya miundombinu ya maji Mkoani Tanga. 

Waziri Ummy amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutatua kero za wananchi wa Mkoa wa Tanga katika Sekta ya Elimu, afya, barabara na maboresho ya Bandari ya Tanga. 

Aidha, Waziri Ummy amesema, Kwa upande wa Sekta ya Afya, Jiji la Tanga lina vituo Sita vya Afya ambavyo vinafanya kazi. 


“Kwa upande wa Hospitali za Rufaa tumesambaza mashine za kisasa za uchunguzi ikiwemo CT-Scan katika Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara ikiwa ni pamoja na hospitali ya Rufaa ya Bombo Tanga". Amesema Waziri Ummy.

Amesema, wananchi wa Mkoa wa Tanga sasa hivi hawana haja ya kwenda tena Dar Es Salaam au Kilimanjaro kwa ajili ya kufata huduma za CT-Scan au huduma za kusafisha damu, huduma zote hizo zinapatikana Mkoani hapo. 

“Hatua hii ni kubwa ambayo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya ya kuwajali wananchi wake katika maendelea na sasa kwenye sekta ya maji Rais Samia atatupatia Bilioni 53 kwa ajili ya mradi wa upatikanaji wa maji kwa asilimia 100 kwa wakazi wa Tanga Mjini pamoja na Wilaya jirani za Muheza na Mkinga". Amesema Waziri Ummy. 

Katika hatua nyingine, Waziri Ummy ametoa rai kwa Watanzania kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi angalau dakika 40 kwa siku mara nne kwa wiki, kupunguza matumizi ya Sukari, Chumvi na Mafuta. 

“Tumeona kuna ongezeko kubwa la magonjwa Yasiyoambukiza ikiwemo Kisukari, shinikizo la Juu la Damu (Presha), na Saratani, ili kupunguza ongezeko la magonjwa hayo lazima tuzingatie mtindo bora wa maisha.” Amesema Waziri na Mbunge wa Tanga Mhe. Ummy Mwalimu.

Mradi huo wa maji uliozinduliwa utazalisha wastani wa jumla ya lita Milioni 60 kutoka lita 45 za awali katika Mkoa wa Tanga.

Post a Comment

0 Comments