Na Mwandishi Wetu,
SINGIDA,
Wilaya ya Iramba imeanza utekelezaji katika kata ya Shelui vijiji vya Nselembwe, Kibigiri na Nkyala. Elimu ya kisheria kuhusiana na masuala ya sheria za ardhi, Mirathi, Ndoa, utawala bora, GBV na ndoa imeweza kutolewa kwa wananchi na baadae huduma ya msaada wa kisheria kwa mtu mmoja mmoja.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupata huduma hiyo Wananchi hao wamesema kuwa wamefurahi sana kwa sababu ni jambo ambalo halijawahi kutokea hivyo Wana kila sababu ya kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali Wananchi wake maeneo mbalimbali Nchini.
“Mimi nimefurahi na kushukuru sana, hivi ninavyoongea ni kwamba nimemuona Mwanasheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria na amenisaidia ina maana suala langu linashughulikiwa natarajia haki itatendeka bila wasiwasi wowote kwa kuwa lipo chini ya usimamizi wa Rais nashukuru sana’’ ameeleza mmoja wa Wananchi hao bwana Salum Juma Saidi.
Mwananchi mwingine Hamad Ramadhani amesema “nilipofika hapa nimeona kuna mabadiliko mambo yote yanafanyika hadharani na watu wote wanasaidiwa, Wanasheria wamenipa hatua nyingine za kufuata ili nipate haki yangu;
Naye Mwananchi Elias Irunde akizungumza kwa niaba ya wenzake amesema "baada ya kusogezewa hii huduma karibu nimeamua nijitokeze kupata huduma nimeona mambo yameenda vizuri’’.
Aidha Malengo ya kampeni hiyo inayoendelea mpaka tarehe 19 Januari 2024 katika Mkoa wa Singida ni kufika katika jumla ya Kata 70 na vijiji 210 vya mkoa huo; hivyo Wananchi wote wa Mkoa huo na maeneo Jirani wametakiwa kuitumia vizuri fursa hiyo kwa kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo yenye kauli mbio isemayo “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa Amani na Maendeleo”
Hata hivyo Kampeni ya hiyo inatokana na Azma ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha kwamba kila mwananchi anafahamu masuala ya kisheria ikiwemo haki na wajibu wake na kwamba kila mwananchi anaifikia haki na wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za mawakili basi waweze kufikia haki kupitia huduma za msaada wa kisheria.
0 Comments