HEADLINES

6/recent/ticker-posts

WADAI WANAPEWA FEDHA NA WANASIASA ILI WASIHAME NGORONGORO


Na Mwandishi Wetu,

KARATU, MANYARA

Baadhi ya Wananchi wanaoishi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wamesema kwamba wamekuwa wakipewa fedha na baadhi ya wanasiasa wa wilaya ya Ngorongoro  ili wasijiandikishe kuhama kwa hiari kwenda maeneo yaliyotengwa na serikali ili waendelee kubaki hifadhini kwa ajili kuchunga mifugo.

Wakizungumza na Mwandishi wetu baadhi ya wananchi hao wanasema kwamba baadhi ya wanasiasa katika eneo hilo wamekuwa wakigawa fedha kwa kupita nyumba kwa nyumba  hasa nyakati za usiku kuwarubuni  na kuwatisha wakatae uamuzi wa kuhama kwa hiari ili wakubaki hifadhini kwa manufaa ya wanasiasa hao.

Mmoja wa wananchi hao (Jina tunalihifadhi kwa usalama wake) alisema alikuwa tayari kuhama lakini mpambe wa mwanasiasa mmoja alimfuata na kumpa shilingi elfu hamsini (50,000) ili akatae kujiandikisha na kuendelea kufanya kazi ya kuchunga  mifugo huku akitishwa kutokubali kujiandikisha.

“Baadhi yetu tunaishi kwa uoga kutokana na vitisho tunavyovipata kutoka kwa baadhi ya viongozi wetu wa kisiasa na wengine wenye ushawishi wa fedha ambao wamekuwa wakitutumia kwa lengo la kuchunga mifugo yao na wengine wanaamini kwamba iwapo tutakubali kuhama watapoteza nafasi zao na hivyo kuamua kusambaza fedha kwa wananchi”,amesema mwananchi huyo.

Mkazi mwingine wa Kijiji cha Bulati tarafa ya Ngorongoro aliyejitambulisha kwa jina la Martin Lenguroi alisema kuwa kwa ujumla kinachowafanya baadhi ya wananchi washindwe kujiandikisha na kutoka hifadhini ni mgao wa fedha wanaoupata kutoka kwa baadhi ya wanasiasa hao ambao wanaamini kwamba iwapo wananchi wataondoka watakosa watu wa kuchunga mifugo yao.


“Ndugu mwandishi wanaoteseka katika eneo hili ni wananchi wa kawaida hasa maskini ambao hawana mifugo, na kinachowaponza ni mgao wa fedha wanaoupata kutoka kwa baadhi ya wanasiasa ili wananchi maskini waendelee kubaki hivyo na wao waendelee kupata watu wa kusimamia mifugo yao, wanasiasa hawa hawana uchungu na wananchi wao wanaangalia maslahi yao tu,”alisema bwana Martin.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika vijiji mbalimbali ndani ya hifadhi hiyo umebaini kuwa katika siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa ya baadhi ya wanasiasa wa wilaya ya Ngorongoro kupita katika vijiji vya tarafa hiyo  kwa kutumia wapambe wao ili kugawa fedha kwa wananchi ambao wengi wao wamekuwa wakiwatumia katika shughuli zao za ufungaji huku wenyewe wakiishi wilayani Karatu na jijini Arusha.

Serikali imekuwa ikiendesha zoezi la kuelimisha, kuhamasisha, kuandikisha na kuwahamasisha wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi waweze kuhama katika maeneo hayo kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi hao kutokana na kuishi katika hali inayotawaliwa na sheria za kulinda hifadhi hivyo kuwafanya wananchi hao kuwa tegemezi na kushindwa kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi.


Post a Comment

0 Comments