Na Amedeus Somi,
DAR ES SALAAM,
Kiongozi wa Kanisa Katoliki
Duniani, Baba Mtakatifu Francis amemualika Rais Samia Suluhu Hassan Mjini
Vatican kwa mazungumzo rasmi ya siku mbili baina ya viongozi hao.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, January Makamba amewaambia waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam
leo kuwa mazungumzo hayo yatafanyika Februari 11 na 12 Vatican nchini Italia.
Makamba amesema kufuatia mwaliko huo, Rais Samia
ameamua kuambatana na waumini wa kawaida wa Katoliki ambao pia wataonana na
Papa Francis katika ziara hiyo ya kihistoria.
"Hii ni heshima kubwa kwa nchi yetu na Rais wetu, kwani mazungumzo hayo na Baba Mtakatifu ni yaheshima kubwa na watu wachache sana ndio watapata fursa ya kuhudhuria mazungumzo hayo," amesema Makamba
DIPLOMASIA YA TANZANIA YAZIDI KUNG’ARA KIMATAIFA
Diplomasia ya Tanzania imezidi kung’ara kimataifa kufuatia viongozi wakuu kutoka mataifa mbalimbali kufanya ziara nchini kwa lengo la kuimarisha na kudumisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na mataifa hayo.Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.), alipozungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam.
Akielezea ziara za viongozi hao nchini Waziri Makamba amesema tarehe 22 Januari 2024 atawasili Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China na Mjumbe wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China, Mhe. Liu Guozhong ambaye atakuwa nchini tarehe 22 - 24 Januari , 2024.
“Mara baada ya kuwasili nchini, kiongozi huyo anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa (Mb.), pamoja na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Dotto Biteko (Mb.),” alisema Waziri Makamba.
Amesema Kiongozi mwingine mkuu anayetarajiwa kuwasili nchini ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Mheshimiwa Salvador Valdes Mesa, ambaye atafanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 23 – 25 Januari, 2024. Pamoja na mambo mengine, ziara hiyo imelenga kuendelea kudumisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Cuba.
Waziri Makamba, amesema Mheshimiwa Mesa anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Husein Ali Mwinyi na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Tulia Akson.
Pamoja na mambo mengine, Mheshimiwa Mesa atamtembelea Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere na kushiriki mkutano wa wanachama wa urafiki kati ya Tanzania na Cuba, Watanzania waliosoma Cuba na Taasisi ya Pan African Movement na kutembelea kiwanda kinachozalisha dawa za viuadudu ya Biolarvicide cha Kibaha, Pwani.
0 Comments