HEADLINES

6/recent/ticker-posts

WAZIRI KAIRUKI AFUNGUA SEMINA YA UMOJA WA WABUNGE WANAWAKE JUMUIYA YA MADOLA

 


Na Mwandishi Wetu, 

DAR ES SALAAM,

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) kwa niaba ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amefungua semina ya Umoja wa Wabunge Wanawake kutoka Mabunge ya Jumuiya ya Madola yenye lengo la kujadili masuala ya usawa wa kijinsia.

Semina hiyo ya siku 3 imeanza leo Desemba 6,2023  jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Hoteli ya Serena.

Amesema semina hiyo pia itajadili pamoja na mambo mengine ni kwa namna gani Mabunge kama chombo cha uwakilishi yanazingatia na yanakuwa na mlengo wa usawa wa kijinsia ,ni kwa namna gani yanakuwa na jicho la usawa wa kijinsia , kuangalia ni namna gani kuna mazingira wezeshi kwa Wabunge wanawake kuweza kutekeleza majukumu yao huku wanaendeleza masuala ya uzazi,na katika uwakilishi wanapewa nafasi kiasi gani za kuweza kuwakilisha wanawake wenzao Bungeni.

Ameongeza kuwa pia majadiliano yatajikita katika kuangalia masuala ya miundombinu, kanuni, sheria, sera mbalimbali kuangalia kuna vikwazo gani vinazuia wanawake wasiweze kushiriki katika nafasi za kisiasa pamoja na uongozi na katika vyombo mbalimbali vya maamuzi.

Mhe. Kairuki ametolea mifano ya nchi zilizofanikiwa kufikia au kuzidi katika masuala ya usawa wa kijinsia kama Australia ambayo kwa muda wa miaka 170 imeweza kupata uwiano wa kijinsia kwa asilimia hamsini kwa hamsini na katika ngazi za maamuzi Baraza la Mawaziri imeweza kufikia wanawake asilimia 67 na wanaume asilimia 33 na nchi ya Rwanda ambayo imefanikiwa kufikia usawa wa kijisia kwa wanawake kwa asilimia 61.


Kwa upande wa Tanzania amesema kwa kuwa inaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwanamke na pia ina Spika wa Bunge ambaye ni Rais wa Mabunge Duniani,  inaelekea kufikia usawa wa kijinsia kwa  asilimia 37 hadi 40 . 

Amefafanua kuwa usawa wa kijinsia katika siasa unaweza kupatikana tu ikiwa wanaume watafanya kazi bega kwa bega na wanawake kushiriki jukumu la kuvunja mila na desturi zenye madhara.

Mkutano huo umehudhuriwa na Wabunge kutoka Mabunge ya Jumuiya ya Madola na  Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Post a Comment

0 Comments