KWA mara ya kwanza Simba itacheza bila mashabiki, mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika raundi ya nne ya hatua ya makundi ya dhidi ya Al Merrikh ya Sudan, mchezo utakaopigwa Machi 16, 2021 Uwanja wa Benjamini Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Uamuzi huo ni mwendelezo wa juhudi za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kukabiliana na maambukizo ya ugonjwa wa Covid-19 ambao umesambaa duniani kote.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara ametangaza leo Jumamosi rasmi kwamba, kupitia kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wamepata taarifa ya kuwataka mechi hiyo, ichezwe bila hata shabiki mmoja kwenda uwanjani, isipokuwa viongozi wa timu zote mbili, TFF na CAF.
"Simba ina miaka 85, haijawahi kutokea kucheza nyumbani bila mashabiki, lakini hakuna namna ya kufanya, jambo la msingi mashabiki wawaombee wachezaji ili waweze kufanya vizuri, maana CAF wakishasema ndio wenye mpira wao, tunakuwa hatuna cha kufanya," amesema na ameongeza kuwa;
"Ingawa kama uongozi wa klabu tunaendelee kulifuatilia hili, kama mechi zinazokuja tunaweza kurudishiwa mashabiki ambao wanakuwa wanawapa nguvu wachezaji wetu, licha ya kwamba wakicheza ugenini wanapambana bila mashabiki," amesema.
Manara amesema japo wanaumia kucheza bila mashabiki wao, wana uhakika wa kufanya vizuri katika mechi hiyo na nyingine ambazo watacheza siku za usoni.
"Simba imeshazoea kucheza mechi bila mashabiki. Tumeshafanya hivyo kule Nigeria, Zimbabwe, DR Congo na hata juzi Sudan na tumefanya vizuri.
Mbali na kwamba mchezo huo wamezuiliwa na CAF kucheza bila ya mashabiki, kama kawaida ya Manara amekuja na kauli mbiu itakayotumika kwenye mchezo huo, aliyoitambulisha kama Silent Killers.
0 Comments